Arca da aliança
A Arca da Aliança era o símbolo mais sagrado de Israel — representava a presença de Deus no meio do seu povo. Sobre ela brilhava a glória do Senhor entre os querubins.
"Nao watatengeneza Sanduku la mbao za mshita, lenye urefu wa dhiraa mbili na nusu, upana wa dhiraa moja na nusu, na kimo cha dhiraa moja na nusu. Utalifunika hilo Sanduku kwa dhahabu safi ndani na nje, na kulifanyia ukingo wa dhahabu juu yake kulizunguka. Utalisubu kwa pete nne za dhahabu na kuzifungia kwenye miguu yake minne, pete mbili kwa upande mmoja na pete mbili kwa upande mwingine. Kisha utatengeneza mipiko ya mti wa mshita na kuzifunika kwa dhahabu. Utaiingiza hiyo mipiko kwenye zile pete katika pande mbili za Sanduku ili kulibeba. Hiyo mipiko itabakia daima katika hizo pete za hilo Sanduku; haitaondolewa. Kisha weka ndani ya hilo Sanduku ule Ushuhuda nitakaokupa.
"Tengeneza kifuniko cha upatanisho cha dhahabu safi, chenye urefu wa dhiraa mbili na nusu, na upana wa dhiraa moja na nusu. Tengeneza makerubi wawili wa dhahabu iliyofuliwa katika miisho ya hicho kifuniko. Tengeneza kerubi mmoja kwenye mwisho mmoja, na kerubi mwingine kwenye mwisho mwingine; watengeneze makerubi hao wawe kitu kimoja na hicho kifuniko katika miisho hiyo miwili. Makerubi hao watakuwa wametandaza mabawa kuelekea juu, yakitia kivuli hicho kifuniko. Makerubi hao wataelekeana, wakitazama hicho kifuniko. Weka huo Ushuhuda nitakaokupa ndani ya hilo Sanduku la Agano, na uweke hicho kifuniko juu ya hilo Sanduku.
Hapo juu ya hicho kifuniko, kati ya hao makerubi wawili walioko juu ya hilo Sanduku la Ushuhuda, hapo ndipo nitakapokutana nawe na kukupa maagizo yangu kwa ajili ya Waisraeli.
Bezaleli akatengeneza Sanduku la mbao za mshita: urefu wake ulikuwa dhiraa mbili na nusu, upana wake dhiraa moja na nusu, na kimo chake dhiraa moja na nusu.
Kisha Bwana akamwambia Mose: "Simika Maskani ya Mungu, yaani Hema la Kukutania, katika siku ya kwanza ya mwezi wa kwanza. Weka Sanduku la Ushuhuda ndani yake na ulifunike kwa pazia. Ingiza meza na kupanga vitu vyake juu yake.
Akachukua ule Ushuhuda na kuuweka ndani ya Sanduku la Agano, akaweka ile mipiko ya kubebea hilo Sanduku na kuweka kiti cha rehema juu yake. Kisha Mose akalileta Sanduku ndani ya Maskani ya Mungu, akatundika pazia ili kulifunika Sanduku la Ushuhuda, kama Bwana alivyomwagiza.
Mose alipoingia kwenye Hema la Kukutania kuzungumza na Bwana, alisikia sauti ikisema naye kutoka kati ya wale makerubi wawili waliokuwa juu ya kile kiti cha rehema, juu ya Sanduku la Ushuhuda. Mose akazungumza naye.
Hivyo waliondoka kutoka mlima wa Bwana, nao wakasafiri kwa siku tatu. Sanduku la Agano la Bwana liliwatangulia kwa zile siku tatu ili kuwatafutia mahali pa kupumzika. Wingu la Bwana lilikuwa juu yao wakati wa mchana walipoondoka kambini.
Wakati wowote Sanduku lilipoondoka, Mose alisema,
"Ee Bwana, inuka!
Watesi wako na watawanyike;
adui zako na wakimbie mbele zako."
Wakati wowote Sanduku liliposimama, alisema,
"Ee Bwana, rudi,
kwa maelfu ya Waisraeli wasiohesabika."
Bwana akamwambia Mose, "Sema na Waisraeli, na ujipatie fimbo kumi na mbili kutoka kwao, moja kutoka kwa kila mmoja wa viongozi wa kabila za baba zao. Andika jina la kila mtu kwenye fimbo yake. Kwenye fimbo ya Lawi andika jina la Aroni, kwa maana ni lazima iwepo fimbo moja kwa kila kiongozi kwa ajili ya kila kabila la baba zao. Ziweke hizo fimbo ndani ya Hema la Kukutania mbele ya Sanduku la Ushuhuda, mahali nikutanapo nawe. Fimbo ya mtu nitakayemchagua itachipuka, nami mwenyewe nitayakomesha haya manungʼuniko ya mara kwa mara ya Waisraeli dhidi yako."
Hivyo Mose akasema na Waisraeli, nao viongozi wao wakampa fimbo kumi na mbili, fimbo moja kwa ajili ya kila kabila la baba zao, nayo fimbo ya Aroni ikiwa miongoni mwa hizo. Mose akaziweka hizo fimbo mbele za Bwana ndani ya Hema la Ushuhuda.
Siku iliyofuata Mose aliingia kwenye Hema la Ushuhuda akaona ile fimbo ya Aroni ambayo iliwakilisha jamaa ya Lawi haikuwa tu imechipuka, bali pia ilikuwa imetoa machipukizi, kuchanua maua na kuzaa malozi. Ndipo Mose akaleta zile fimbo zote kwa Waisraeli wote kutoka mbele za Bwana. Wakaziangalia, na kila mtu akaichukua fimbo yake mwenyewe.
Bwana akamwambia Mose, "Rudisha fimbo ya Aroni mbele ya Sanduku la Ushuhuda, ili ihifadhiwe kama alama kwa waasi. Hili litakomesha manungʼuniko yao dhidi yangu, ili kwamba wasife." Mose akafanya kama Bwana alivyomwamuru.
Basi, watu walipovunja kambi ili kuvuka Yordani, makuhani wakiwa wamebeba Sanduku la Agano waliwatangulia. Wakati huu ulikuwa wakati wa mavuno, nao Mto Yordani ulikuwa umefurika hadi kwenye kingo zake. Ilikuwa kawaida ya Yordani kufurika nyakati zote za mavuno. Mara tu makuhani wale waliokuwa wamebeba Sanduku la Agano walipofika mtoni na nyayo zao kuzama ndani ya yale maji, maji hayo yaliyotiririka kutoka upande wa juu yaliacha kutiririka yakasimama kama chuguu mbali kabisa nao, kwenye mji ulioitwa Adamu kwenye eneo la Sarethani, wakati yale maji yaliyokuwa yanatiririka kuingia kwenye Bahari ya Araba (yaani Bahari ya Chumvi), yalitindika kabisa. Hivyo watu wakavuka kukabili Yeriko.
Wale makuhani waliobeba Sanduku la Agano la Bwana, wakasimama imara mahali pakavu katikati ya Mto Yordani, wakati Waisraeli wote wakiwa wanapita hadi taifa lote likaisha kuvuka mahali pakavu.
Nao makuhani wakapanda kutoka ndani ya Mto Yordani wakilibeba hilo Sanduku la Agano la Bwana. Mara tu walipoiweka miguu yao penye kingo, nje ya mto, maji ya Yordani yakarudi kufurika kama ilivyokuwa kabla.
Basi malango ya Yeriko yalifungwa kwa uthabiti kwa ajili ya Waisraeli. Hakuna mtu yeyote aliyetoka au kuingia.
Kisha Bwana akamwambia Yoshua, "Tazama, nimeitia Yeriko mikononi mwako, pamoja na mfalme wake na watu wake wa vita. Zunguka mji mara moja pamoja na watu wote wenye silaha. Fanya hivi kwa siku sita. Uwe na makuhani saba wakibeba mabaragumu ya pembe za kondoo dume mbele ya Sanduku. Siku ya saba, mzunguke mji mara saba, nao makuhani wakipiga baragumu hizo. Utakapowasikia wamepaliza sauti kubwa ya baragumu, watu wote wapige kelele kwa sauti kuu, kisha ukuta wa mji utaanguka na watu watapanda, kila mtu akiendelea mbele."
Ndipo Yoshua mwana wa Nuni akaita makuhani na kuwaambia, "Chukueni Sanduku la Agano la Bwana na makuhani saba wachukue baragumu za pembe za kondoo dume mbele yake." Naye akawaagiza watu, "Songeni mbele! Mkauzunguke mji, na walinzi wenye silaha watangulie mbele ya Sanduku la Bwana."
Wakati baragumu zilipopigwa, watu walipiga kelele, na katika sauti ya baragumu, na watu kupaza sauti, ukuta ukaanguka; hivyo kila mtu akapanda akiendelea mbele na kuuteka mji.
Wafilisti wakapanga safu za majeshi yao kupambana na Israeli, wakati vita vilipoenea, Israeli wakashindwa na Wafilisti, ambao waliwaua askari wa Israeli wapatao 4,000 kwenye uwanja wa vita. Askari waliporudi kambini, wazee wa Israeli wakawauliza, "Kwa nini Bwana ameruhusu leo tushindwe mbele ya Wafilisti? Tuleteni Sanduku la Agano la Bwana kutoka Shilo, ili lipate kwenda pamoja nasi, na kutuokoa kutoka mikono ya adui zetu."
Hivyo wakawatuma watu huko Shilo, nao wakalichukua Sanduku la Agano la Bwana Mwenye Nguvu Zote, aliyekaa kwenye kiti chake cha enzi kati ya makerubi. Nao wale wana wawili wa Eli, Hofni na Finehasi, walikuwako huko pamoja na Sanduku la Agano la Mungu.
Wakati Sanduku la Agano la Bwana lilikuja kambini, Waisraeli wote wakapiga kelele kwa sauti kuu hata ardhi ikatikisika. Wafilisti waliposikia makelele wakauliza, "Ni nini makelele haya yote katika kambi ya Waebrania?"
Walipofahamu kuwa Sanduku la Bwana limekuja kambini, Wafilisti wakaogopa, wakasema, "Mungu amekuja kambini, ole wetu. Halijatokea jambo kama hili tangu hapo. Ole wetu! Ni nani atakayetuokoa kutoka mikononi mwa miungu hii yenye nguvu? Ni miungu ile iliyowapiga Wamisri kwa mapigo ya aina zote huko jangwani. Tuweni hodari, enyi Wafilisti! Tuweni wanaume, la sivyo mtakuwa watumwa wa Waebrania, kama wao walivyokuwa kwenu. Kuweni wanaume, mpigane!"
Basi Wafilisti wakapigana, nao Waisraeli wakashindwa na kila mtu akakimbilia hemani mwake. Mauaji yalikuwa makubwa sana, Israeli wakapoteza askari 30,000 waendao kwa miguu. Sanduku la Mungu likatekwa, na hao wana wawili wa Eli, Hofni na Finehasi, wakauawa.
Mkono wa Bwana ulikuwa mzito juu ya watu wa Ashdodi na vijiji jirani, akaleta uharibifu juu yao na kuwatesa kwa majipu. Watu wa Ashdodi walipoona kile kilichokuwa kikitokea, wakasema, "Sanduku la Mungu wa Israeli kamwe lisikae hapa pamoja na sisi, kwa sababu mkono wake ni mzito juu yetu na juu ya Dagoni mungu wetu." Basi wakawaita watawala wote wa Wafilisti pamoja na kuwauliza, "Tutafanya nini na hili Sanduku la Mungu wa Israeli?"
Wakajibu, "Sanduku la Mungu wa Israeli na liende Gathi." Basi wakalihamisha Sanduku la Mungu wa Israeli.
Lakini baada ya kulihamisha, mkono wa Bwana ulikuwa dhidi ya huo mji wa Gathi, akiuweka katika fadhaa kuu. Mungu akawatesa watu wa huo mji, vijana kwa wazee, kwa kuwaletea majipu. Basi wakapeleka Sanduku la Mungu Ekroni.
Wakati Sanduku la Mungu lilipokuwa linaingia Ekroni, watu wa Ekroni walilia wakisema "Wamelileta Sanduku la Mungu wa Israeli kwetu ili kutuua sisi na watu wetu." Basi wakawaita watawala wote wa Wafilisti pamoja na kusema, "Liondoeni Sanduku la Mungu wa Israeli na lirudishwe mahali pake, la sivyo litatuua sisi na watu wetu." Kwa kuwa kifo kilikuwa kimeujaza mji hofu; kwani mkono wa Mungu ulikuwa mzito sana juu yake.
Sanduku la Bwana lilipokuwa limekaa katika nchi ya Wafilisti kwa miezi saba, Wafilisti waliwaita makuhani wa Dagoni na waaguzi, na kuwaambia, "Tutafanya nini na hili Sanduku la Bwana? Tuambieni jinsi tutakavyolirudisha mahali pake."
Wakajibu, "Kama mtalirudisha Sanduku la Mungu wa Israeli, msilirudishe mikono mitupu bali kwa vyovyote mpelekeeni sadaka ya hatia. Kisha mtaponywa, nanyi mtafahamu kwa nini mkono wake haujaondolewa kwenu."
Basi wakafanya hivyo. Wakachukua ngʼombe wawili wa aina hiyo, wakawafungia hilo gari la kukokotwa, nao ndama wao wakawekwa zizini. Wakaliweka Sanduku la Bwana juu ya hilo gari la kukokotwa pamoja na lile kasha lenye ile mifano ya panya wa dhahabu na ya majipu ya dhahabu. Kisha hao ngʼombe wakaenda moja kwa moja kuelekea Beth-Shemeshi, wakishuka bila kugeuka kuume au kushoto, huku wakilia njia yote. Watawala wa Wafilisti waliwafuata hao ngʼombe hadi mpakani mwa Beth-Shemeshi.
Wakati huu watu wa Beth-Shemeshi walikuwa wakivuna ngano yao huko bondeni, walipoinua macho yao na kuona lile Sanduku, wakafurahi kuliona. Lile gari la kukokotwa lilikuja mpaka kwenye shamba la Yoshua wa Beth-Shemeshi, nalo likasimama kando ya mwamba mkubwa. Watu wakapasua mbao za lile gari la kukokotwa na kutoa dhabihu wale ngʼombe kama sadaka ya kuteketezwa kwa Bwana. Walawi walilishusha Sanduku la Bwana, pamoja na lile kasha lililokuwa na vile vitu vya dhahabu na kuviweka juu ya ule mwamba mkubwa. Siku ile watu wa Beth-Shemeshi wakatoa sadaka za kuteketezwa na dhabihu kwa Bwana.
Kisha watu wa Kiriath-Yearimu wakaja na kulichukua Sanduku la Bwana. Wakalipeleka katika nyumba ya Abinadabu juu kilimani na kumweka Eleazari mwanawe wakfu kulichunga Sanduku la Bwana.
Sanduku la Bwana lilibakia huko Kiriath-Yearimu kwa muda mrefu, yaani jumla ya miaka ishirini, nao watu wa Israeli wakaomboleza na kumtafuta Bwana.
Kisha Mfalme Daudi akaambiwa, "Bwana ameibariki nyumba ya Obed-Edomu pamoja na kila alicho nacho, kwa sababu ya Sanduku la Mungu." Basi Daudi akateremka na kulipandisha Sanduku la Mungu kutoka nyumba ya Obed-Edomu hadi Mji wa Daudi kwa shangwe. Wale waliokuwa wamebeba Sanduku la Bwana walipokuwa wametembea hatua sita, Daudi alitoa dhabihu fahali na ndama aliyenoneshwa. Daudi, akiwa amevaa kisibau cha kitani, alicheza mbele za Bwana kwa nguvu zake zote, wakati yeye na nyumba yote ya Israeli walipopandisha Sanduku la Bwana kwa shangwe na sauti za tarumbeta.
Kisha Mfalme Solomoni akawaita mbele zake huko Yerusalemu wazee wa Israeli, viongozi wote wa makabila na wakuu wa jamaa za Waisraeli, ili walilete Sanduku la Agano la Bwana kutoka Sayuni, Mji wa Daudi. Wanaume wote wa Israeli wakakusanyika kwa Mfalme Solomoni wakati wa sikukuu ya mwezi wa Ethanimu, ndio mwezi wa saba.
Wazee wote wa Israeli walipofika, makuhani wakajitwika Sanduku la Agano, nao wakalipandisha Sanduku la Bwana, na Hema la Kukutania pamoja na vyombo vyote vitakatifu vilivyokuwa ndani yake. Makuhani na Walawi wakavibeba, naye Mfalme Solomoni na kusanyiko lote la Israeli waliokusanyika kumzunguka walikuwa mbele ya hilo Sanduku, nao wakatoa dhabihu nyingi za kondoo na ngʼombe ambao idadi yao haikuwezekana kuandikwa au kuhesabiwa.
Makuhani wakalileta Sanduku la Agano la Bwana hadi mahali pake ndani ya sehemu takatifu ndani ya Hekalu, yaani Patakatifu pa Patakatifu, na kuliweka chini ya mabawa ya makerubi. Makerubi yalitandaza mabawa yao juu ya mahali pa Sanduku la Agano na kutia kivuli Sanduku pamoja na mipiko yake ya kubebea. Mipiko hiyo ilikuwa mirefu sana kiasi kwamba ncha zake zilionekana kutoka Mahali Patakatifu mbele ya Patakatifu pa Patakatifu, lakini sio nje ya Mahali Patakatifu. Hiyo mipiko ipo hata leo. Ndani ya Sanduku hapakuwepo kitu kingine chochote isipokuwa zile mbao mbili za mawe ambazo Mose alikuwa ameziweka ndani yake huko Horebu, mahali ambapo Bwana alifanya Agano na Waisraeli baada ya kutoka Misri.
Makuhani walipoondoka katika Mahali Patakatifu, wingu likajaza Hekalu la Bwana. Nao makuhani hawakuweza kufanya huduma yao kwa sababu ya lile wingu, kwa kuwa utukufu wa Bwana ulijaza Hekalu lake.
"Rudini, enyi watu msio waaminifu, kwa kuwa mimi ni mume wenu," asema Bwana. "Nitawachagua ninyi, mmoja kutoka kwenye mji, na wawili kutoka kwenye ukoo, nami nitawaleta Sayuni. Kisha nitawapeni wachungaji wanipendezao moyo wangu, ambao watawaongoza kwa maarifa na ufahamu. Katika siku hizo, idadi yenu itakapokuwa imeongezeka sana katika nchi, watu hawatasema tena, ‘Sanduku la Agano la Bwana,’ " asema Bwana. "Halitaingia tena kwenye mawazo yao wala kukumbukwa, hawatalihitaji wala halitatengenezwa jingine.
Basi agano lile la kwanza lilikuwa na kanuni zake za kuabudu na pia patakatifu pake pa kidunia. Hema ilitengenezwa. Katika sehemu yake ya kwanza kulikuwa na kinara cha taa, meza na mikate iliyowekwa wakfu; hii sehemu iliitwa Mahali Patakatifu. Nyuma ya pazia la pili, palikuwa na sehemu iliyoitwa Patakatifu pa Patakatifu, ambapo palikuwa na yale madhabahu ya dhahabu ya kufukizia uvumba, na lile Sanduku la Agano lililofunikwa kwa dhahabu. Sanduku hili lilikuwa na gudulia la dhahabu lenye mana, ile fimbo ya Aroni iliyochipuka, na vile vibao vya mawe vya Agano. Juu ya lile Sanduku kulikuwa na makerubi ya Utukufu yakitilia kivuli kile kifuniko ambacho ndicho kiti cha rehema. Lakini hatuwezi kueleza vitu hivi kwa undani sasa.
Ndipo hekalu la Mungu lililoko mbinguni likafunguliwa, na sanduku la agano lake likaonekana humo ndani. Kukatokea mianga ya umeme wa radi, ngurumo, sauti za radi, tetemeko la nchi na mvua kubwa ya mawe.