Publicidade

Arca da aliança

Por Bíblia Online

A Arca da Aliança era o símbolo mais sagrado de Israel — representava a presença de Deus no meio do seu povo. Sobre ela brilhava a glória do Senhor entre os querubins.

Sanduku la Agano

Nao na wafanye sanduku la mti wa mjohoro; urefu wake na uwe dhiraa mbili na nusu, na upana wake dhiraa moja na nusu, na kwenda juu kwake dhiraa moja na nusu. Nawe ulifunike kwa dhahabu safi, ulifunike ndani na nje, nawe tia na ukingo wa dhahabu kulizunguka pande zote. Nawe subu vikuku vinne vya dhahabu kwa ajili yake, na kuvitia katika miguu yake minne; vikuku viwili upande mmoja, na vikuku viwili upande wake wa pili. Nawe fanya miti mirefu ya mshita na kuifunika dhahabu. Nawe tia hiyo miti katika vile vikuku vilivyo katika pande mbili za sanduku ili kulichukua hilo sanduku. Hiyo miti itakaa katika vile vikuku vya sanduku; haitaondolewa. Kisha tia ndani ya sanduku huo ushuhuda nitakaokupa. Nawe fanya kiti cha rehema cha dhahabu safi; urefu wake utakuwa dhiraa mbili na nusu, na upana wake dhiraa moja na nusu. Nawe fanya makerubi mawili ya dhahabu; uyafanye ya kazi ya kufua, katika hiyo miisho ya kiti cha rehema, huku na huku. Weka kerubi moja mwisho mmoja, na kerubi la pili mwisho wa pili; fanya hayo makerubi yawe kitu kimoja na kiti cha rehema, mwisho huku na mwisho huku. Na hayo makerubi yatainua mabawa yao juu, na kukifunika hicho kiti cha rehema kwa mabawa yao, na nyuso zao zitaelekeana hili na hili; nyuso za hayo makerubi zitaelekea kiti cha rehema. Weka kiti cha rehema juu ya hilo sanduku, kisha utie huo ushuhuda nitakaokupa ndani ya sanduku.

Nami nitaonana nawe hapo, na kuzungumza nawe pale nilipo juu ya kiti cha rehema, katikati ya hayo makerubi mawili yaliyo juu ya sanduku la ushuhuda, katika mambo yote nitakayokuagiza kwa ajili ya wana wa Israeli.

Kutengeneza sanduku la Agano

Kisha Bezaleli akalifanya lile sanduku la mti wa mshita, urefu wake ulikuwa dhiraa mbili na nusu, na upana wake ulikuwa dhiraa moja na nusu, na kwenda juu kwake kulikuwa ni dhiraa moja na nusu;

Hema lasimikwa na vifaa vyake kuwekwa wakfu

BWANA akanena na Musa, na kumwambia, Siku ya kwanza ya mwezi wa kwanza utaisimamisha hiyo maskani ya hema ya kukutania. Nawe utatia ndani yake sanduku la ushuhuda, nawe utalisitiri hilo sanduku kwa pazia.

Akautwaa ule ushuhuda, akautia ndani ya sanduku, akaiweka miti ya kuchukulia juu ya sanduku, akakiweka kiti cha rehema juu ya sanduku; kisha akalileta sanduku akalitia ndani ya maskani, naye akalitundika pazia la sitara, akalisitiri sanduku la ushuhuda; kama BWANA alivyomwamuru Musa.

Kisha, Musa alipoingia ndani ya hema ya kukutania ili kunena na Mungu ndipo alipoisikia Sauti ikinena naye kutoka hapo juu ya kiti cha rehema, kilichokuwa juu ya sanduku la ushahidi, ikitoka kati ya yale makerubi mawili; naye akanena naye.

Basi wakasafiri kutoka penye mlima wa BWANA safari ya siku tatu; na sanduku la Agano la BWANA likatangulia mbele yao mwendo wa siku tatu, ili kuwatafutia mahali pa kupumzika. Na wingu la BWANA lilikuwa juu yao mchana hapo waliposafiri kwenda mbele kutoka kambini.

Ilikuwa, hapo sanduku liliposafiri kwenda mbele, ndipo Musa akasema, Inuka, Ee BWANA, adui zako na watawanyike; na wakimbie mbele zako hao wakuchukiao. Tena hapo liliposimama, akasema, Ee BWANA, uwarudie maelfu kumi ya maelfu ya Israeli.

Kuchipuka kwa fimbo ya Haruni

Kisha BWANA akanena na Musa, akamwambia, Nena na wana wa Israeli, kisha upokee kwao fimbo, fimbo moja kwa ajili ya nyumba ya kila baba, katika wakuu wao wote, kama nyumba za baba zao zilivyo, fimbo kumi na mbili; kisha andika jina la kila mtu katika fimbo yake. Na katika fimbo ya Lawi utaliandika jina la Haruni; maana, itakuwa fimbo moja kwa kila kichwa cha nyumba za baba zao. Nawe utaziweka katika hema ya kukutania mbele ya huo ushahidi, hapo nikutanapo pamoja nanyi. Kisha itakuwa, mtu huyo nitakayemchagua, fimbo yake itachipuka nami nitayakomesha manung’uniko ya wana wa Israeli, wanung’unikiayo kwangu juu yenu. Basi Musa akawaambia wana wa Israeli, ndipo wakuu wao wote wakampa fimbo, fimbo moja kwa kila mkuu, kama nyumba za baba zao zilivyokuwa, fimbo kumi na mbili; na fimbo ya Haruni ilikuwa kati ya fimbo zao. Kisha Musa akaziweka hizo fimbo mbele za BWANA katika hema ya kukutania. Ilikuwa siku ya pili yake, Musa akaingia ndani ya hema ya ushahidi; na tazama, ile fimbo ya Haruni iliyokuwa kwa nyumba ya Lawi ilikuwa imechipuka, imetoa michipukizi, na kuchanua maua; na kuzaa matunda mabivu. Kisha Musa akazitoa nje hizo fimbo zote kutoka hapo mbele za BWANA na kuziweka mbele ya wana wa Israeli wote; nao wakaangalia, na kila mtu akaitwaa fimbo yake. Kisha BWANA akamwambia Musa, Irudishe fimbo ya Haruni mbele ya ushahidi, ili itunzwe iwe ishara juu ya hawa wana wa maasi; ili uyakomeshe manung’uniko yao waliyoninung’unikia, ili wasife. Basi Musa akafanya hivyo; kama BWANA alivyomwagiza, ndivyo alivyofanya.

Hata ikawa, hao watu walipotoka katika hema zao, ili kuvuka Yordani, makuhani waliolichukua sanduku la Agano wakatangulia mbele ya watu, basi hao waliolichukua hilo sanduku walipofika Yordani, na nyayo za makuhani waliolichukua sanduku zilipotiwa katika maji ya ukingoni, (maana Yordani hujaa hata kingo zake na kufurika wakati wote wa mavuno), ndipo hayo maji yaliyoshuka kutoka juu yakasimama, yakainuka, yakawa kichuguu, mbali sana, huko Adamu, mji ule ulio karibu na Sarethani, na maji yale yaliyoteremkia bahari ya Araba, yaani Bahari ya Chumvi, yataacha kutiririka kabisa; watu wakavuka kukabili Yeriko. Na hao makuhani waliolichukua sanduku la Agano la BWANA wakasimama imara mahali pakavu katikati ya Yordani; Israeli wote wakavuka katika nchi kavu, hadi taifa lile lote likaisha kuvuka Yordani.

Ilikuwa, hapo hao makuhani waliolichukua sanduku la Agano la BWANA walipokwea juu kutoka mle kati ya Yordani, na nyayo za miguu yao hao makuhani zilipoinuliwa na kutiwa katika nchi kavu, ndipo maji ya Yordani yaliporudi mahali pake, na kufurika katika kingo zake zote, kama yalivyokuwa hapo kwanza.

Yeriko watwaliwa na kuangamizwa

Basi Yeriko ulikuwa umefungwa kabisa kwa sababu ya Waisraeli; hapana mtu aliyetoka wala hapana mtu aliyeingia. BWANA akamwambia Yoshua, Tazama, nimeutia Yeriko katika mkono wako, na mfalme wake, na mashujaa wake. Nanyi mtauzunguka mji huu, wapiganaji wote, mkiuzunguka mji mara moja. Fanya hivi siku sita. Na makuhani saba watachukua baragumu saba za pembe za kondoo dume, watatangulia mbele za hilo sanduku; na siku ya saba mtauzunguka mji mara saba, nao makuhani watapiga baragumu zao. Kisha itakuwa watakapopiga hizo pembe za kondoo dume kwa nguvu, nanyi mtakaposikia kwa mlio wa baragumu, watu wote watapiga kelele kwa sauti kuu; na ukuta wa mji utaanguka chini pale pale, na hao watu watapanda, kila mtu akiendelea mbele kukabili. Bali Yoshua, mwana wa Nuni, akawaita makuhani, akawaambia, Lichukueni sanduku la Agano, tena makuhani saba na wachukue mabaragumu saba za pembe za kondoo dume watangulie mbele ya sanduku la BWANA. Naye akawaambia watu, Piteni mbele, mkauzunguke mji, na hao watu wenye silaha na watangulie mbele ya sanduku la BWANA.

Basi watu wakapiga kelele, na makuhani wakazipiga tarumbeta; hata ikawa, hapo watu waliposikia mlio wa mabaragumu hao watu wakapiga kelele kwa sauti kuu sana, na ule ukuta wa mji ukaanguka chini kabisa, hata watu wakapanda juu, wakaingia katika mji, kila mtu akisonga mbele kukabili; wakautwaa huo mji.

Nao Wafilisti wakajipanga juu ya Israeli; na walipopigana, Waisraeli wakapigwa na Wafilisti; waliowaua karibu elfu nne katika uwanja wa vita. Hata watu walipofika kambini, wazee wa Israeli wakasema, Mbona BWANA ametupiga leo mbele ya Wafilisti? Twende tukalilete sanduku la Agano la BWANA kutoka Shilo hadi huku, lije kati yetu, na kutuokoa katika mikono ya adui zetu. Basi wakatuma watu kwenda Shilo, nao wakalileta toka huko sanduku la Agano la BWANA wa majeshi, akaaye juu ya makerubi; na Hofni na Finehasi, wana wawili wa Eli, walikuwako huko pamoja na sanduku la Agano la Mungu. Na sanduku la Agano la BWANA lilipoingia kambini, Israeli wote wakapiga kelele kwa sauti kuu, hata nchi ikavuma. Nao Wafilisti waliposikia mshindo wa zile kelele, walisema, Maana yake nini mshindo wa kelele hizi kubwa katika kambi ya Waebrania? Wakatambua ya kuwa sanduku la BWANA limefika kambini. Wafilisti wakaogopa, maana walisema, Mungu ameingia kambini. Wakasema, Ole wetu! Kwani halijawa jambo kama hili tangu hapo. Ole wetu! Ni nani anayeweza kutuokoa kutoka kwa miungu hawa wenye nguvu? Hawa ndio miungu waliowapiga Wamisri kwa mapigo ya kila namna jangwani. Jipeni moyo, na kufanya kiume enyi Wafilisti, msije mkawa watumwa wa Waebrania, kama wao walivyokuwa watumwa wenu; fanyeni kiume, mkapigane nao. Wafilisti wakapigana nao, Israeli wakapigwa, wakakimbia kila mtu hemani kwake; wakauawa watu wengi sana; maana katika Israeli walianguka watu elfu thelathini walioenda vitani kwa miguu. Hilo sanduku la Mungu likatwaliwa; na Hofni na Finehasi, wale wana wawili wa Eli, wakauawa.

Lakini mkono wa BWANA ulikuwa mzito juu ya watu wa Ashdodi, akawaangamiza, akawapiga kwa majipu, huko Ashdodi na mipakani mwake. Kisha hao watu wa Ashdodi, walipoona ilivyokuwa, walisema, Hilo sanduku la Mungu wa Israeli halitakaa kwetu; kwa maana mkono wake ni mzito juu yetu, na juu ya Dagoni, mungu wetu. Basi wakatuma watu waende kuwakusanya kwao wakuu wote wa Wafilisti, wakasema, Tulifanyieje sanduku la Mungu wa Israeli? Nao wakajibu, Sanduku la Mungu wa Israeli na lihamishwe liende Gathi. Wakalihamisha sanduku la Mungu wa Israeli. Ikawa, walipolihamisha, mkono wa BWANA ulikuwa juu ya mji huo, kwa kuwafadhaisha sana; akawapiga watu wa mjini, wadogo kwa wakubwa, wakapatwa na majipu. Basi, wakalipeleka sanduku la Mungu mpaka Ekroni. Ikawa, sanduku la Mungu lilipofika Ekroni, watu wa Ekroni walipiga kelele, wakasema, Wamelileta hilo sanduku la Mungu wa Israeli kwetu, ili kutuua sisi na watu wetu. Kwa hiyo wakatuma watu waende kuwakusanya wakuu wote wa Wafilisti, wakasema, Liondoeni hilo sanduku la Mungu wa Israeli, liende tena mahali pake, ili lisituue sisi, wala watu wetu; kwa sababu kulikuwa na fadhaa kubwa sana mjini kote; mkono wa Mungu ulikuwa mzito mno huko.

Sanduku la Agano larudishwa Israeli

Basi, hilo sanduku la BWANA lilikuwamo katika nchi ya Wafilisti muda wa miezi saba. Nao Wafilisti wakawaita makuhani na waaguzi, wakasema, Tulifanyieje sanduku la BWANA? Tuonesheni jinsi tuwezavyo kulirudisha mahali pake. Nao wakajibu, Mkilirudisha hilo sanduku la Mungu wa Israeli, msilirudishe kitupu; lakini msikose kumpelekea na matoleo ya kosa; hivyo mtapona, tena mtafunuliwa ni kwa sababu gani mkono wake haukuondolewa kwenu.

Basi watu wale walifanya hivyo; wakatwaa ng’ombe wawili wakamuliwao, wakawafunga garini, na ndama wao wakawafunga zizini; kisha wakaliweka sanduku la BWANA juu ya gari, pamoja na kasha lenye panya wa dhahabu na sanamu za majipu yao. Na hao ng’ombe wakashika njia moja kwa moja kwenda Beth-shemeshi; wakaiandama njia ya barabara, wakaenda wakilia, lakini hawakugeukia upande wa kulia wala wa kushoto; na wakuu wa Wafilisti wakawafuata hata kuufikia mpaka wa Beth-shemeshi. Nao watu wa Beth-shemeshi walikuwa wakivuna ngano yao bondeni; wakainua macho yao, wakaliona sanduku, wakafurahi sana kuliona. Na lile gari likaingia katika konde la Yoshua wa Beth-shemeshi, na kusimama pale pale, palipokuwapo jiwe kubwa; basi wakaipasua miti ya lile gari, wakawatoa wale ng’ombe kuwa ni sadaka ya kuteketezwa kwa BWANA. Nao Walawi walilishusha sanduku la BWANA, na lile kasha lililokuwa pamoja nalo, lenye vile vitu vya dhahabu; wakaviweka juu ya lile jiwe kubwa; nao watu wa Beth-shemeshi wakatoa sadaka za kuteketezwa, na kuchinja dhabihu siku iyo hiyo kwa BWANA.

Na hao watu wa Kiriath-yearimu wakaja, wakalichukua sanduku la BWANA, wakalipeleka ndani ya nyumba ya Abinadabu huko kilimani, nao wakamtenga Eleazari, mwanawe, ili alilinde sanduku la BWANA.

Ikawa, tangu sanduku lipelekwe Kiriath-yearimu, muda mrefu ulipita; maana ulikuwa miaka ishirini; na nyumba yote ya Waisraeli wakamwombolezea BWANA.

Kisha mfalme Daudi akaambiwa ya kwamba, BWANA ameibariki nyumba ya Obed-edomu, na vitu vyote alivyo navyo kwa ajili ya sanduku la Mungu. Daudi akaenda, akalileta sanduku la Mungu, toka nyumba ya Obed-edomu mpaka mji wa Daudi, kwa shangwe. Hata ikawa, watu waliolichukua sanduku la BWANA walipokwisha kwenda hatua sita, akachinja fahali na ndama mnono. Daudi akacheza mbele za BWANA kwa nguvu zake zote; na Daudi alikuwa amevaa naivera ya kitani. Basi Daudi na nyumba yote ya Israeli wakalileta sanduku la BWANA kwa shangwe, na kwa sauti ya tarumbeta.

Hekalu kuwekwa wakfu

Ndipo Sulemani alipowakusanya wazee wa Israeli, na wakuu wote wa makabila na wakuu wa koo za wana wa Israeli, wamwendee mfalme Sulemani huko Yerusalemu, ili walipandishe sanduku la Agano la BWANA kutoka mji wa Daudi, yaani, Sayuni. Watu wote wa Israeli wakakutana mbele ya mfalme Sulemani wakati wa sikukuu, katika mwezi wa Ethanimu, ndio mwezi wa saba. Wazee wote wa Israeli wakaja, nao makuhani wakajitwika sanduku. Wakalipandisha sanduku la BWANA, na ile hema ya kukutania, na vyombo vitakatifu vyote vilivyokuwa katika ile Hema; vitu hivyo makuhani na Walawi wakavipandisha. Mfalme Sulemani, na mkutano wote wa Israeli waliokutanika kwake, walikuwako pamoja naye mbele ya sanduku, wakichinja sadaka kondoo na ng’ombe, wasioweza kuhesabiwa wala idadi yao kujulikana kwa kuwa wengi.

Makuhani wakalileta sanduku la Agano la BWANA hadi mahali pake, katika chumba cha ndani cha ile nyumba, patakatifu pa patakatifu, naam, chini ya mbawa za makerubi. Kwa maana makerubi yalinyosha mbawa zao, juu ya mahali pa sanduku, makerubi yakalifunika lile sanduku na miti yake kwa juu. Na ile miti kwa kuwa mirefu, ncha za miti zilionekana katika mahali patakatifu, mbele ya chumba cha ndani; lakini hazikuonekana nje; nayo iko kuko huko hata leo. Hamkuwa na kitu ndani ya sanduku, ila zile mbao mbili za mawe ambazo Musa aliziweka ndani huko Horebu, BWANA alipofanya agano na wana wa Israeli, hapo walipotoka katika nchi ya Misri. Ikawa, makuhani walipotoka katika patakatifu, nyumba ya BWANA ikajaa wingu; hata makuhani hawakuweza kusimama ili kufanya huduma yao, kwa sababu ya wingu lile; kwa kuwa nyumba ya BWANA ilikuwa imejaa utukufu wa BWANA.

Rudini, enyi watoto wenye kuasi, asema BWANA; maana mimi ni mume wenu; nami nitatwaa mtu mmoja wa mji mmoja, na wawili wa jamaa moja, nami nitawaleta hadi Sayuni; nami nitawapa ninyi wachungaji wanipendezao moyo wangu, watakaowalisha kwa maarifa na fahamu. Kisha itakuwa, mtakapoongezeka na kuwa wengi katika nchi hiyo, asema BWANA, siku zile hawatasema tena, Sanduku la Agano la BWANA; wala halitaingia moyoni; wala hawatalikumbuka, wala hawatalizuru, wala hayatafanyika hayo tena.

Maskani ya duniani na ya mbinguni

Basi hata agano la kwanza lilikuwa na kawaida za ibada, na patakatifu pake, pa kidunia. Maana hema ilitengenezwa, ile ya kwanza, mlimokuwa na kinara cha taa, na meza, na mikate mitakatifu; ndipo palipoitwa, Patakatifu. Na nyuma ya pazia la pili, ile hema iitwayo Patakatifu pa patakatifu, yenye chetezo cha dhahabu, na sanduku la Agano lililofunikwa kwa dhahabu pande zote, mlimokuwa na kopo la dhahabu lenye ile mana, na ile fimbo ya Haruni iliyochipuka, na vile vibao vya agano; na juu yake makerubi ya utukufu, yakikitia kivuli kiti cha rehema; basi hatuna nafasi sasa ya kueleza habari za vitu hivi kimoja kimoja.

Kisha hekalu la Mungu lililoko mbinguni likafunguliwa, na sanduku la Agano lake likaonekana ndani ya hekalu lake. Kukawa na umeme, na sauti, na radi, na tetemeko la nchi, na mvua kubwa ya mawe.

Seja o primeiro
Bíblia Online Bíblia Online

Bíblia Online • Versão: 2026-07-05_19-25-13-