Maombi Ya Hana
1 Kisha Hana akaomba na kusema:
"Moyo wangu wamshangilia Bwana,
katika Bwana pembe yangu imeinuliwa juu.
Kinywa changu chajisifu juu ya adui zangu,
kwa kuwa naufurahia wokovu wako.
2 "Hakuna yeyote aliye mtakatifu kama Bwana,
hakuna mwingine zaidi yako;
hakuna Mwamba kama Mungu wetu.
3 "Msiendelee kusema kwa kiburi hivyo
wala msiache vinywa vyenu kunena kwa kiburi,
kwa kuwa Bwana ndiye Mungu ajuaye,
na kwa yeye matendo hupimwa.
4 "Pinde za mashujaa zimevunjika,
lakini wale wanaojikwaa wamevikwa nguvu.
5 Wale waliokuwa na chakula tele wamejikodisha wenyewe
ili kupata chakula,
lakini wale waliokuwa na njaa
hawana njaa tena.
Mwanamke yule aliyekuwa tasa
amezaa watoto saba,
lakini yule ambaye alikuwa na wana wengi
amedhoofika.
6 "Bwana huua na huleta uhai,
hushusha chini mpaka kaburini2:6 Kaburini hapa maana yake ni Kuzimu, kwa Kiebrania ni Sheol. na hufufua.
7 Bwana humfanya mtu maskini naye hutajirisha,
hushusha na hukweza.
8 Humwinua maskini kutoka mavumbini
na humwinua mhitaji kutoka lundo la majivu;
huwaketisha pamoja na wakuu
na kuwafanya warithi kiti cha enzi cha heshima.
"Kwa kuwa misingi ya dunia ni ya Bwana;
juu yake ameuweka ulimwengu.
9 Yeye atailinda miguu ya watakatifu wake,
lakini waovu watanyamazishwa kwenye giza.
"Si kwa nguvu mtu hushinda;
10 wale wampingao Bwana
wataharibiwa kabisa.
Atapiga radi dhidi yao kutoka mbinguni;
Bwana ataihukumu miisho ya dunia.
"Atampa nguvu mfalme wake,
na kuitukuza pembe
ya mpakwa mafuta wake."