Wana Waovu Wa Eli
12 Wana wa Eli walikuwa watu wabaya kabisa, hawakumheshimu Bwana. 13 Basi ilikuwa desturi ya makuhani pamoja na watu kwamba kila mara yeyote anapotoa dhabihu na huku nyama ikiwa inachemshwa, mtumishi wa kuhani angalikuja na uma wenye meno matatu mkononi mwake. 14 Angeutumbukiza huo uma kwenye sufuria au birika au sufuria kubwa au chungu, naye kuhani angalijichukulia mwenyewe chochote ambacho uma ungekileta. Hivi ndivyo walivyowatendea Waisraeli wote waliokuja Shilo. 15 Lakini hata kabla mafuta ya mnyama hayajachomwa, mtumishi wa kuhani angalikuja na kusema kwa mtu ambaye alikuwa akitoa dhabihu, "Mpe kuhani nyama akaoke, kwani hatapokea nyama iliyochemshwa kutoka kwako, ila iliyo mbichi tu."
16 Kama mtu akimwambia, "Mafuta ya mnyama na yachomwe kwanza, ndipo uchukue chochote unachotaka," mtumishi angalijibu, "Hapana, nipe sasa, kama huwezi nitaichukua kwa nguvu."
17 Hii Dhambi ya hawa vijana ilikuwa kubwa sana machoni pa Bwana, kwa kuwa waliitendea dhabihu ya Bwana kwa dharau.