2 Wafilisti wakapanga safu za majeshi yao kupambana na Israeli, wakati vita vilipoenea, Israeli wakashindwa na Wafilisti, ambao waliwaua askari wa Israeli wapatao 4,000 kwenye uwanja wa vita. 3 Askari waliporudi kambini, wazee wa Israeli wakawauliza, "Kwa nini Bwana ameruhusu leo tushindwe mbele ya Wafilisti? Tuleteni Sanduku la Agano la Bwana kutoka Shilo, ili lipate kwenda pamoja nasi, na kutuokoa kutoka mikono ya adui zetu."
4 Hivyo wakawatuma watu huko Shilo, nao wakalichukua Sanduku la Agano la Bwana Mwenye Nguvu Zote, aliyekaa kwenye kiti chake cha enzi kati ya makerubi. Nao wale wana wawili wa Eli, Hofni na Finehasi, walikuwako huko pamoja na Sanduku la Agano la Mungu.
5 Wakati Sanduku la Agano la Bwana lilikuja kambini, Waisraeli wote wakapiga kelele kwa sauti kuu hata ardhi ikatikisika. 6 Wafilisti waliposikia makelele wakauliza, "Ni nini makelele haya yote katika kambi ya Waebrania?"
Walipofahamu kuwa Sanduku la Bwana limekuja kambini, 7 Wafilisti wakaogopa, wakasema, "Mungu amekuja kambini, ole wetu. Halijatokea jambo kama hili tangu hapo. 8 Ole wetu! Ni nani atakayetuokoa kutoka mikononi mwa miungu hii yenye nguvu? Ni miungu ile iliyowapiga Wamisri kwa mapigo ya aina zote huko jangwani. 9 Tuweni hodari, enyi Wafilisti! Tuweni wanaume, la sivyo mtakuwa watumwa wa Waebrania, kama wao walivyokuwa kwenu. Kuweni wanaume, mpigane!"
10 Basi Wafilisti wakapigana, nao Waisraeli wakashindwa na kila mtu akakimbilia hemani mwake. Mauaji yalikuwa makubwa sana, Israeli wakapoteza askari 30,000 waendao kwa miguu. 11 Sanduku la Mungu likatekwa, na hao wana wawili wa Eli, Hofni na Finehasi, wakauawa.