Mungu Wa Faraja Yote
3 Ahimidiwe Mungu na Baba wa Bwana wetu Yesu Kristo, Baba wa huruma na Mungu wa faraja yote. 4 Yeye hutufariji katika taabu zetu, ili tuweze kuwafariji walio katika taabu yoyote kwa faraja ambayo sisi wenyewe tumepokea kutoka kwa Mungu. 5 Kama vile mateso ya Kristo yanavyozidi ndani ya maisha yetu, hivyo ndivyo faraja yetu inavyofurika kwa njia ya Kristo. 6 Kama tunataabika, ni kwa ajili ya faraja na wokovu wenu; kama tukifarijiwa, ni kwa ajili ya faraja yenu, iwaleteayo saburi ya mateso yale yale yanayotupata. 7 Nalo tumaini letu kwenu ni thabiti, kwa sababu tunajua kwamba kama vile mnavyoshiriki mateso yetu, ndivyo pia mnavyoshiriki katika faraja yetu.