Pular para o conteúdo
Publicidade

2 Wafalme 4

Mwana Wa Mshunami Afufuliwa

8 Siku moja Elisha akaenda Shunemu. Huko kulikuwa na mwanamke mmoja mwenye cheo, ambaye alimsisitiza Elisha aje kula chakula. Kwa hiyo kila mara alipitia pale, akaingia humo ili ale. 9 Akamwambia mumewe, "Ninajua kwamba huyu mtu ambaye anakuja kwetu mara kwa mara ni mtu mtakatifu wa Mungu. 10 Tutengeneze chumba kidogo juu darini na tuweke ndani yake kitanda na meza, kiti na taa kwa ajili yake. Kisha anaweza kukaa humo kila mara akija kwetu."

11 Siku moja Elisha alipofika, akapanda chumbani kwake na kulala humo. 12 Akamwambia mtumishi wake Gehazi, "Mwite huyo Mshunami." Hivyo akamwita, naye akaja akasimama mbele yake. 13 Elisha akamwambia mtumishi wake, "Mwambie huyu mwanamke, Umetaabika sana kwa ajili yetu. Sasa utendewe nini? Je, tunaweza kuzungumza na mfalme au jemadari wa jeshi kwa niaba yako?’ "

Akajibu, "Mimi ninaishi kwangu miongoni mwa watu wangu."

14 Elisha akamwambia mtumishi wake, "Je, ni nini kinachoweza kufanyika kwa ajili yake?"

Gehazi akasema, "Hakika, hana mwana, na mume wake ni mzee."

15 Ndipo Elisha akasema, "Mwite huyo mwanamke." Kwa hiyo akamwita, naye akaja akasimama mlangoni. 16 Elisha akamwambia, "Mwaka ujao, wakati kama huu utabeba mwana mikononi mwako."

Yule mama akapinga, akasema, "La hasha, bwana wangu, usimpotoshe mtumishi wako, ee mtu wa Mungu!"

17 Lakini yule mwanamke akapata mimba, na mwaka uliofuata wakati kama ule ule akamzaa mwana, kama vile Elisha alivyokuwa amemwambia.

18 Mtoto akakua, naye siku moja akamwendea baba yake, ambaye alikuwa pamoja na wavunaji. 19 Akamwambia baba yake, "Kichwa changu! Kichwa changu!"

Baba yake akamwambia mtumishi, "Mchukue umpeleke kwa mama yake." 20 Baada ya mtumishi kumbeba na kumpeleka kwa mama yake, mtoto akaketi mapajani mwa mama yake mpaka adhuhuri, kisha akafa. 21 Mama akampandisha na kumlaza juu ya kitanda cha yule mtu wa Mungu, kisha akafunga mlango, akatoka nje.

22 Akamwita mume wake na kusema, "Tafadhali mtume mmoja miongoni mwa mtumishi pamoja na punda ili niweze kwenda kwa mtu wa Mungu haraka na kurudi."

23 Mume wake akamuuliza, "Kwa nini uende kwake leo? Leo si mwandamo wa mwezi, wala si Sabato."

Mwanamke akasema, "Yote ni sawa."

24 Akatandika punda na kumwambia mtumishi wake, "Mwongoze huyo punda. Usinipunguzie mwendo mpaka nikuambie." 25 Kwa hiyo akaenda na kumfikia huyo mtu wa Mungu katika Mlima Karmeli.

Alipomwona kwa mbali, huyo mtu wa Mungu akamwambia mtumishi wake Gehazi, "Tazama, yule Mshunami! 26 Kimbia ukamlaki, umuulize, Je, wewe hujambo? Mume wako hajambo? Mtoto wako ni mzima?’ "

Akasema, "Kila kitu ni sawasawa."

27 Alipomfikia huyo mtu wa Mungu pale mlimani, akashika miguu yake. Gehazi akaja ili amwondoe, lakini yule mtu wa Mungu akasema, "Mwache! Yuko katika uchungu mkubwa, lakini Bwana amenificha jambo hili na hajaniambia kwa nini."

28 Yule mwanamke akasema, "Je, bwana wangu, mimi nilikuomba mwana? Je, sikukuambia, Usiamshe matumaini yangu?"

29 Elisha akamwambia Gehazi, "Jikaze viuno, chukua fimbo yangu mkononi mwako na ukimbie. Ikiwa utakutana na mtu yeyote, usimsalimie, na mtu yeyote akikusalimu, usimjibu. Ilaze fimbo yangu juu ya uso wa mtoto."

30 Lakini mama mtoto akasema, "Hakika kama Bwana aishivyo na wewe uishivyo, sitakuacha." Kwa hiyo Elisha akainuka, akafuatana naye.

31 Gehazi akatangulia mbele na kuilaza fimbo juu ya uso wa mtoto, lakini hapakuwa na sauti wala itikio. Hivyo Gehazi akarudi kukutana na Elisha, na kumwambia, "Mtoto hajaamka."

32 Elisha alipofika kwenye ile nyumba, mtoto alikuwa amelala juu ya kitanda chake angali amekufa. 33 Akaingia ndani, akajifungia yeye na yule mtoto, akamwomba Bwana. 34 Kisha akapanda kitandani, akalala juu ya yule mtoto, mdomo wake juu ya mdomo wa mtoto, macho yake juu ya macho ya mtoto, mikono yake juu ya mikono ya mtoto. Naye alipojinyoosha juu yake, mwili wa mtoto ukapata joto. 35 Elisha akajiondoa juu yake na kuanza kutembeatembea ndani ya chumba, kisha akarudi tena kitandani na kujinyoosha tena juu ya mtoto mara nyingine. Mtoto akapiga chafya mara saba, akafungua macho yake.

36 Elisha akamwita Gehazi na kumwambia, "Mwite huyo Mshunami." Naye akafanya hivyo. Yule Mshunami alipokuja, Elisha akasema, "Mchukue mwanao." 37 Akaingia ndani, akaanguka miguuni pa Elisha na kusujudu hadi nchi. Kisha akamchukua mwanawe na kutoka nje.

Veja também