Pigo La Tano: Vifo Vya Mifugo
1 Ndipo Bwana akamwambia Mose, "Nenda kwa Farao ukamwambie, ‘Hili ndilo Bwana, Mungu wa Waebrania asemalo: "Waachie watu wangu waende ili wapate kuniabudu." 2 Kama ukikataa kuwaachia waende, nawe ukiendelea kuwashikilia, 3 mkono wa Bwana utaleta pigo baya kwa mifugo yako, juu ya farasi wako, punda, ngamia, ngʼombe wako, kondoo na mbuzi. 4 Lakini Bwana ataweka tofauti kati ya mifugo ya Israeli na ile ya Misri, kwamba hakuna mnyama wa Mwisraeli atakayekufa.’ "
5 Bwana akaweka wakati na kusema, "Kesho Bwana atalitenda hili katika nchi." 6 Siku iliyofuata Bwana akalitenda: Mifugo yote ya Wamisri ikafa, lakini hakuna hata mnyama mmoja wa wana wa Israeli aliyekufa. 7 Farao akatuma watu kuchunguza, nao wakakuta kuwa hakuna hata mnyama mmoja wa Waisraeli aliyekufa. Lakini moyo wa Farao haukukubali kuwaachia watu waende.