3 Abramu akaanguka kifudifudi, naye Mungu akamwambia, 4 "Kwa upande wangu, hili ndilo Agano langu na wewe: Wewe utakuwa baba wa mataifa mengi. 5 Jina lako hutaitwa tena Abramu, bali jina lako litakuwa Abrahamu, kwa maana nimekufanya wewe baba wa mataifa mengi. 6 Nitakufanya uwe na uzao mwingi sana, kwako yatatoka mataifa nao wafalme watatoka kwako. 7 Nitalithibitisha Agano langu kama Agano la milele kati yangu na wewe na wazao wako baada yako na vizazi vijavyo niwe Mungu wako na Mungu wa wazao wako. 8 Nchi yote ya Kanaani, unakoishi sasa kama mgeni, nitakupa kuwa milki yako milele, na uzao wako, nami nitakuwa Mungu wao."
9 Ndipo Mungu akamwambia Abrahamu, "Kwa upande wako, lazima ushike Agano langu, wewe na wazao wako kwa ajili ya vizazi vijavyo. 10 Hili ni Agano langu na wewe pamoja na wazao wako baada yako, Agano mtakalolishika: Kila mwanaume miongoni mwenu atatahiriwa. 11 Mtafanyiwa tohara na hii itakuwa ni alama ya Agano kati yangu na ninyi.