1 Basi agano lile la kwanza lilikuwa na kanuni zake za kuabudu na pia patakatifu pake pa kidunia. 2 Hema ilitengenezwa. Katika sehemu yake ya kwanza kulikuwa na kinara cha taa, meza na mikate iliyowekwa wakfu; hii sehemu iliitwa Mahali Patakatifu. 3 Nyuma ya pazia la pili, palikuwa na sehemu iliyoitwa Patakatifu pa Patakatifu, 4 ambapo palikuwa na yale madhabahu ya dhahabu ya kufukizia uvumba, na lile Sanduku la Agano lililofunikwa kwa dhahabu. Sanduku hili lilikuwa na gudulia la dhahabu lenye mana, ile fimbo ya Aroni iliyochipuka, na vile vibao vya mawe vya Agano. 5 Juu ya lile Sanduku kulikuwa na makerubi ya Utukufu yakitilia kivuli kile kifuniko ambacho ndicho kiti cha rehema. Lakini hatuwezi kueleza vitu hivi kwa undani sasa.
Publicidade
Publicidade