Unabii Wa Zekaria
67 Zekaria, baba yake, akajazwa na Roho Mtakatifu, naye akatoa unabii, akisema:
68 "Ahimidiwe Bwana, Mungu wa Israeli,
kwa kuwa amewajilia watu wake na kuwakomboa.
69 Naye ametusimamishia pembe1:69 Pembe hapa inamaanisha nguvu. ya wokovu
katika nyumba ya Daudi mtumishi wake,
70 kama alivyonena kwa vinywa vya manabii
wake watakatifu tangu zamani,
71 kwamba atatuokoa kutoka kwa adui zetu,
na kutoka mikononi mwao wote watuchukiao:
72 ili kuonyesha rehema kwa baba zetu
na kukumbuka Agano lake takatifu,
73 kiapo alichomwapia baba yetu Abrahamu:
74 kutuokoa kutoka mikononi mwa adui zetu,
tupate kumtumikia yeye pasipo hofu
75 katika utakatifu na haki mbele zake,
siku zetu zote.
76 "Nawe mtoto wangu, utaitwa nabii wa Aliye Juu Sana;
kwa kuwa utamtangulia Bwana
na kuandaa njia kwa ajili yake,
77 kuwajulisha watu wake juu ya wokovu
utakaopatikana kwa kusamehewa dhambi zao,
78 kwa ajili ya wingi wa rehema za Mungu wetu,
nuru itokayo juu itatuzukia
79 ili kuwaangazia wale waishio gizani
na katika uvuli wa mauti,
kuiongoza miguu yetu katika njia ya amani."