Zakayo Mtoza Ushuru
1 Yesu akaingia Yeriko, naye alikuwa anapita katikati ya huo mji. 2 Tazama, palikuwa na mtu mmoja mkuu wa watoza ushuru naye alikuwa tajiri, jina lake Zakayo. 3 Yeye alikuwa akijitahidi kumwona Yesu ni mtu wa namna gani. Lakini kutokana na umati mkubwa wa watu hakuweza kwa sababu alikuwa mfupi wa kimo. 4 Kwa hiyo akatangulia mbio mbele ya umati wa watu akapanda juu ya mkuyu ili amwone Yesu, kwa sababu angeipitia njia ile.
5 Yesu alipofika pale chini ya huo mkuyu, akatazama juu, akamwambia, "Zakayo, shuka upesi, kwa maana leo nitakuwa mgeni nyumbani kwako!" 6 Hivyo Zakayo akashuka upesi, akamkaribisha Yesu nyumbani kwake kwa furaha kubwa.
7 Watu wote walipoona hivyo, wakaanza kunungʼunika wakisema, "Amekwenda kuwa mgeni wa ‘mtu mwenye dhambi.’ "
8 Lakini Zakayo akasimama na kumwambia Bwana, "Tazama, Bwana! Sasa hivi nusu ya mali yangu ninawapa maskini, nami kama nimemdhulumu mtu yeyote kitu chochote, nitamrudishia mara nne ya hicho kiwango."
9 Ndipo Yesu akamwambia, "Leo, wokovu umeingia nyumbani humu, kwa sababu huyu naye ni mwana wa Abrahamu. 10 Kwa maana Mwana wa Adamu amekuja kutafuta na kuokoa kile kilichopotea."