Petro Amkana Yesu
54 Kisha wakamkamata Yesu, wakamchukua, wakaenda naye mpaka nyumbani kwa kuhani mkuu. Lakini Petro akafuata kwa mbali. 55 Walipokwisha kuwasha moto katikati ya ua na kuketi pamoja, Petro naye akaketi pamoja nao. 56 Mtumishi mmoja wa kike akamwona kwa mwanga wa moto akiwa ameketi pale. Akamtazama sana, akasema, "Huyu mtu pia alikuwa pamoja na Yesu!"
57 Lakini Petro akakana, akasema, "Ewe mwanamke, hata simjui!"
58 Baadaye kidogo, mtu mwingine alimwona Petro akasema, "Wewe pia ni mmoja wao!" Petro akajibu, "Wewe mtu, mimi sio mmoja wao!"
59 Baada ya muda wa kama saa moja hivi, mtu mwingine akazidi kusisitiza, "Kwa hakika huyu mtu naye alikuwa pamoja na Yesu, kwa maana yeye pia ni Mgalilaya."
60 Petro akajibu, "Wewe mtu, mimi sijui unalosema!" Wakati huo huo, akiwa bado anazungumza, jogoo akawika. 61 Naye Bwana akageuka, akamtazama Petro. Ndipo Petro akakumbuka lile neno ambalo Bwana alimwambia: "Kabla jogoo hajawika leo, utanikana mara tatu." 62 Naye akaenda nje, akalia kwa majonzi.