Yesu Ajaribiwa Na Shetani
1 Yesu, akiwa amejaa Roho Mtakatifu, akarudi kutoka Yordani. Akaongozwa na Roho Mtakatifu hadi nyikani, 2 mahali ambako kwa siku arobaini alikuwa akijaribiwa na ibilisi. Kwa siku zote hizo hakula chochote, hivyo baada ya muda huo akaona njaa.
3 Ibilisi akamwambia, "Ikiwa wewe ni Mwana wa Mungu, amuru jiwe hili liwe mkate."
4 Yesu akajibu akamwambia, "Imeandikwa: ‘Mtu haishi kwa mkate tu.’ "
5 Ibilisi akampeleka hadi juu ya mlima mrefu akamwonyesha milki zote za dunia kwa mara moja. 6 Akamwambia, "Nitakupa mamlaka juu ya milki hizi na fahari zake zote, kwa maana zimekabidhiwa mkononi mwangu nami ninaweza kumpa yeyote ninayetaka. 7 Hivyo ikiwa utanisujudia na kuniabudu, vyote vitakuwa vyako."
8 Yesu akamjibu, "Imeandikwa: ‘Mwabudu Bwana Mungu wako na umtumikie yeye peke yake.’ "
9 Kisha ibilisi akampeleka mpaka Yerusalemu, akamweka juu ya mnara mrefu wa Hekalu, akamwambia, "Kama wewe ndiwe Mwana wa Mungu, jitupe chini kutoka hapa, 10 kwa maana imeandikwa:
" ‘Atakuagizia malaika zake
ili wakulinde;
11 nao watakuchukua mikononi mwao,
usije ukajikwaa mguu wako katika jiwe.’ "
12 Yesu akamjibu, "Imesemwa, ‘Usimjaribu Bwana Mungu wako.’ "
13 Ibilisi alipomaliza kila jaribu, akamwacha Yesu mpaka wakati mwingine ufaao.
Mwanzo Wa Huduma Ya Galilaya
(Mathayo 4:12-17; Marko 1:14-15)