Yesu Aingia Yerusalemu Kwa Shangwe
1 Walipokaribia Yerusalemu, wakafika Bethfage na Bethania katika Mlima wa Mizeituni. Yesu akawatuma wawili wa wanafunzi wake, 2 akawaambia, "Nendeni katika kijiji kilichoko mbele yenu. Na hapo mtakapoingia kijijini, mtamkuta mwana-punda amefungwa hapo, ambaye hajapandwa na mtu bado. Mfungueni, mkamlete hapa. 3 Kama mtu yeyote akiwauliza, ‘Mbona mnamfungua?’ Mwambieni, ‘Bwana anamhitaji, na atamrudisha hapa baada ya muda mfupi.’ "
4 Wakaenda, wakamkuta mwana-punda amefungwa kando ya barabara, karibu na mlango wa nyumba. 5 Walipokuwa wanamfungua, watu waliokuwa wamesimama karibu wakawauliza, "Mna maana gani mnapomfungua huyo mwana-punda?" 6 Wakawajibu kama vile Yesu alivyokuwa amewaagiza, nao wale watu wakawaruhusu. 7 Kisha wakamleta huyo mwana-punda kwa Yesu na kutandika mavazi yao juu yake, naye akampanda.