24 Ndipo Yesu akaondoka hapo akaenda sehemu za Tiro. Akaingia katika nyumba moja, naye hakutaka mtu yeyote ajue kwamba yuko humo. Lakini hakuweza kujificha. 25 Mara mwanamke mmoja, ambaye binti yake mdogo alikuwa na pepo mchafu, akaja na kumpigia magoti miguuni pake. 26 Basi huyo mwanamke alikuwa Myunani, aliyezaliwa Foinike ya Siria.7:26 Kulikuwa na Foinike ya Siria (ndio Shamu) na Foinike ya Libya. Akamsihi Yesu amtoe binti yake huyo pepo mchafu.
27 Yesu akamwambia, "Waache watoto washibe kwanza, kwa maana si vyema kuchukua chakula cha watoto na kuwatupia mbwa."
28 Lakini yule mwanamke akamjibu, "Bwana, hata mbwa walio chini ya meza hula makombo ya chakula cha watoto."
29 Ndipo Yesu akamjibu, "Kwa sababu ya jibu lako, nenda zako nyumbani; yule pepo mchafu amemtoka binti yako."
30 Akaenda zake nyumbani akamkuta binti yake amelala kitandani, yule pepo mchafu akiwa amemtoka.