Yesu Abadilika Sura Mlimani
1 Siku sita baada ya jambo hili, Yesu akawachukua Petro, Yakobo na Yohana ndugu yake Yakobo, akawapeleka juu ya mlima mrefu peke yao. 2 Wakiwa huko, Yesu alibadilika sura mbele yao. Uso wake ukangʼaa kama jua na nguo zake zikawa na weupe wa kuumiza macho. 3 Ghafula wakawatokea mbele yao Mose na Eliya, wakizungumza na Yesu.
4 Ndipo Petro akamwambia Yesu, "Bwana, ni vyema sisi tukae hapa. Ukitaka, nitafanya vibanda vitatu: kimoja chako, kingine cha Mose na kingine cha Eliya."
5 Petro alipokuwa angali ananena, ghafula wingu lililongʼaa likawafunika, na sauti ikatoka kwenye hilo wingu ikisema, "Huyu ni Mwanangu mpendwa. Ninapendezwa naye sana. Msikieni yeye."