Yohana Mbatizaji Atayarisha Njia
1 Siku hizo Yohana Mbatizaji alikuja akihubiri katika nyika ya Uyahudi, akisema, 2 "Tubuni, kwa maana Ufalme wa Mbinguni umekaribia." 3 Huyu ndiye yule aliyenenwa habari zake na nabii Isaya aliposema:
"Sauti ya mtu aliaye huko nyikani,
‘Tayarisheni njia kwa ajili ya Bwana,
yanyoosheni mapito yake.’ "
4 Basi Yohana alivaa mavazi yaliyotengenezwa kwa singa za ngamia, akiwa na mkanda wa ngozi kiunoni mwake. Chakula chake kilikuwa nzige na asali ya mwitu. 5 Watu walikuwa wakimwendea kutoka Yerusalemu, Uyahudi yote na nchi zote za kandokando ya Mto Yordani. 6 Nao wakaziungama dhambi zao, akawabatiza katika Mto Yordani.