Kujaribiwa Kwa Yesu
1 Kisha Yesu akaongozwa na Roho Mtakatifu kwenda nyikani ili akajaribiwe na ibilisi. 2 Baada ya kufunga siku arobaini usiku na mchana, hatimaye akaona njaa. 3 Mjaribu akamjia na kumwambia, "Ikiwa wewe ndiye Mwana wa Mungu, amuru mawe haya yawe mikate."
4 Lakini Yesu akajibu, "Imeandikwa: ‘Mtu haishi kwa mkate tu, ila kwa kila neno litokalo katika kinywa cha Mungu.’ "
5 Ndipo ibilisi akamchukua Yesu mpaka mji mtakatifu na kumweka juu ya mnara mrefu wa Hekalu, 6 akamwambia, "Kama wewe ndiwe Mwana wa Mungu jitupe chini. Kwa kuwa imeandikwa:
" ‘Atakuagizia malaika zake,
nao watakuchukua mikononi mwao
ili usije ukajikwaa mguu wako katika jiwe.’ "
7 Yesu akamjibu, "Pia imeandikwa: ‘Usimjaribu Bwana Mungu wako.’ "
8 Kwa mara nyingine, ibilisi akamchukua Yesu mpaka kwenye kilele cha mlima mrefu na kumwonyesha falme zote za dunia na fahari zake, 9 kisha akamwambia, "Nitakupa hivi vyote kama ukinisujudia na kuniabudu."
10 Yesu akamwambia, "Ondoka mbele yangu, Shetani! Kwa maana imeandikwa, ‘Mwabudu Bwana Mungu wako, na umtumikie yeye peke yake.’ "
11 Ndipo ibilisi akamwacha, nao malaika wakaja na kumhudumia.