14 Zaidi ya hayo, kutoka mwaka wa ishirini wa Mfalme Artashasta, wakati nilipoteuliwa kuwa mtawala wao katika nchi ya Yuda, mpaka mwaka wake wa thelathini na mbili, yaani miaka kumi na miwili, mimi wala ndugu zangu hatukula chakula ambacho kwa kawaida hupewa watawala. 15 Lakini watawala wa mwanzoni, wale walionitangulia, waliwalemea watu na kuchukua kutoka kwao shekeli arobaini za fedha,5:15 Shekeli 40 za fedha ni sawa na gramu 456. pamoja na chakula na mvinyo. Wasaidizi wao pia walijifanya wakuu juu ya watu. Lakini kwa kumheshimu Mungu sikufanya hivyo. 16 Badala yake, nilijitoa kwa bidii katika kazi ya ukuta huu. Watu wangu wote walikutanika pale kwa ajili ya kazi. Hatukujipatia shamba lolote.
17 Zaidi ya hayo, Wayahudi na maafisa 150 walikula mezani pangu, pamoja na wale waliotujia kutoka mataifa jirani. 18 Kila siku niliandaliwa maksai mmoja, kondoo sita wazuri, na kuku, na mvinyo wa kila aina kwa wingi kila baada ya siku kumi. Licha ya mambo haya yote, sikudai chakula kilichokuwa fungu la mtawala, kwa sababu madai yalikuwa mazito sana kwa watu hawa.
19 Unikumbuke kwa fadhili, Ee Mungu wangu, kwa yote niliyofanya kwa ajili ya watu hawa.