1 Mtu ajitengaye na wengine
hufuata matakwa yake mwenyewe;
hupiga vita kila shauri jema.
2 Mpumbavu hafurahii ufahamu,
bali hufurahia kutangaza
maoni yake mwenyewe.
3 Wakati uovu unapokuja, dharau huja pia,
pamoja na aibu huja lawama.
4 Maneno ya kinywa cha mwanadamu ni kina cha maji,
bali chemchemi ya hekima ni kijito kinachobubujika.
5 Sio vizuri kumpendelea mtu mwovu,
au kumnyima haki asiye na hatia.
6 Midomo ya mpumbavu humletea ugomvi
na kinywa chake hualika kipigo.
7 Kinywa cha mpumbavu ni uharibifu wake
na midomo yake ni mtego kwa nafsi yake.
8 Maneno ya mchongezi ni kama chakula kitamu;
huingia sehemu za ndani sana za mtu.
9 Mtu aliye mlegevu katika kazi yake
ni ndugu na yule anayeharibu.
10 Jina la Bwana ni ngome imara,
wenye haki huikimbilia na kuwa salama.
11 Mali ya tajiri ni mji wake wenye ngome,
wanaudhania kuwa ukuta usioweza kurukwa.
12 Kabla ya anguko moyo wa mtu hujaa kiburi,
bali unyenyekevu hutangulia heshima.
13 Yeye ajibuye kabla ya kusikiliza,
huo ni upumbavu wake na aibu yake.
14 Roho ya mtu itastahimili katika ugonjwa
bali roho iliyovunjika ni nani awezaye kuistahimili?