Maneno Ya Mwisho: Mke Mwenye Sifa Nzuri
10 Mke mwenye sifa nzuri, ni nani awezaye kumpata?
Yeye ni wa thamani sana kuliko marijani.31:10 imetungwa kila mstari ukianzia na herufi ya alfabeti ya Kiebrania zikifuatana tangu Aleph (A) hadi Taw (T); zote ni 22.
11 Mume wake anamwamini kikamilifu
wala hakosi kitu chochote cha thamani.
12 Humtendea mumewe mema, wala si mabaya,
siku zote za maisha yake.
13 Huchagua sufu na kitani
naye hufanya kazi kwa mikono yenye bidii.
14 Yeye ni kama meli za biashara
akileta chakula chake kutoka mbali.
15 Yeye huamka kungali bado giza
huwapa jamaa yake chakula
na mafungu kwa watumishi wake wa kike.
16 Huangalia shamba na kulinunua,
kutokana na mapato yake hupanda shamba la mizabibu.
17 Hufanya kazi zake kwa nguvu,
mikono yake ina nguvu kwa ajili ya kazi zake.
18 Huona kwamba biashara yake ina faida,
wala taa yake haizimiki usiku.
19 Huweka mikono yake kwenye pia,
navyo vidole vyake hushikilia kijiti chenye uzi.
20 Huwanyooshea maskini mikono yake
na kuwakunjulia wahitaji vitanga vyake.