Maagizo kuhusu ndoa
1 Basi kuhusu mambo yale mliyoandika, ni heri mwanamume asimguse mwanamke. 2 Lakini kwa sababu ya zinaa kila mwanamume na awe na mke wake mwenyewe, na kila mwanamke na awe na mume wake mwenyewe. 3 Mume na ampe mkewe haki yake, na vivyo hivyo mke na ampe mumewe haki yake. 4 Mke hana amri juu ya mwili wake, bali mumewe; vivyo hivyo mume hana amri juu ya mwili wake, bali mkewe. 5 Msinyimane isipokuwa mmepatana kwa muda, ili mpate faragha kwa kusali; mkarudiane tena, Shetani asije akawajaribu kwa kutokuwa na kiasi kwenu.