1 1 Pet 5:1;3 Yoh 1:1 Mzee, kwa mama mteule na watoto wake niwapendao katika kweli; wala si mimi peke yangu, bali na wote waijuayo ile kweli; 2 kwa ajili ya hiyo kweli ikaayo ndani yetu, nayo itakuwa pamoja nasi hata milele. 3 Neema, na rehema, na amani, zitokazo kwa Mungu Baba na kwa Yesu Kristo Mwana wa Baba, zitakuwa pamoja nasi katika kweli na upendo.
4 Nilifurahi mno kwa kuwa nimewaona baadhi ya watoto wako wanaenenda katika kweli, kama vile tulivyopokea amri kwa Baba. 5 Yn 13:34;15:12,17;1 Yoh 2:7 Na sasa mama, nakuomba, si kwamba nakuandikia amri mpya, bali ile tuliyokuwa nayo tangu mwanzo, kwamba tupendane. 6 Na huu ndio upendo: tuenende kwa kuzifuata amri zake. Hii ndiyo ile amri, kama mlivyosikia tangu mwanzo kwamba mwenende kwayo. 7 1 Yoh 2:18;4:1-3 Kwa maana wadanganyifu wengi wametokea duniani, wasiokiri ya kuwa Yesu Kristo yuaja katika mwili. Huyo ndiye yule mdanganyifu na mpinga Kristo. 8 Gal 4:11 Jiangalieni nafsi zenu msiyapoteze mliyoyatenda, bali mpokee thawabu timilifu. 9 1 Yoh 2:23 Kila apitaye cheo, wala asidumu katika mafundisho ya Kristo, yeye hana Mungu. Yeye adumuye katika mafundisho hayo, huyo ana Baba na Mwana pia. 10 2 The 3:6;1 Fal 13:17;3 Yoh 1:8 Mtu akija kwenu, naye haleti mafundisho hayo, msimkaribishe nyumbani mwenu, wala msimpe salamu. 11 Maana yeye ampaye salamu azishiriki kazi zake mbovu.
12 3 Yoh 1:13 Kwa kuwa ninayo mambo mengi, sitaki kuyaandika kwa karatasi na wino; lakini natarajia kuja kwenu, na kusema nanyi uso kwa uso, ili furaha yetu iwe imetimizwa. 13 Watoto wa dada yako aliye mteule, wakusalimu.