1 Lisikieni neno hili, enyi ng’ombe wa Bashani, mnaokaa juu ya mlima wa Samaria, mnaowaonea maskini, na kuwaponda wahitaji; mnaowaambia bwana zao, Haya! Leteni, tunywe. 2 Bwana MUNGU ameapa kwa utakatifu wake, ya kuwa, tazama, siku zitawajia, watakapowaondoa ninyi kwa kulabu, na mabaki yenu kwa ndoana. 3 Nanyi mtatoka kwenye mahali palipobomolewa, kila mwanamke moja kwa moja mbele yake; nanyi mtajitupa katika Harmoni, asema BWANA.
4 Eze 20:39;Hos 4:15;Hes 28:3,4 Njooni Betheli, mkakose; njoni Gilgali, mkaongeze makosa; kaleteni dhabihu zenu kila asubuhi, na zaka zenu kila siku ya tatu; 5 Kum 12:6 mkachome sadaka ya shukrani, ya kitu kilichotiwa chachu; mkatangaze sadaka mtoazo kwa hiari na kuzihubiri habari zake; kwa maana ndivyo viwapendezavyo ninyi, enyi wana wa Israeli, asema Bwana MUNGU.
6 1 Fal 17:1;Isa 9:13;Yer 5:3;Hos 5:15;Hag 2:17 Mimi nami nimewapa usafi wa meno katika miji yenu yote, na kutindikiwa na mkate mahali penu pote; lakini hamkunirudia mimi, asema BWANA. 7 Tena nimeizuia mvua msiipate, ilipobaki miezi mitatu kabla ya mavuno; nami nimenyesha mvua juu ya mji mmoja, nikaizuia mvua isinyeshe juu ya mji mwingine; sehemu moja ilipata mvua, na sehemu isiyopata mvua ilikauka. 8 Basi kutoka miji miwili mitatu walitangatanga kuendea mji mwingine wapate kunywa maji, wasipate ya kuwatosha; lakini hamkunirudia mimi, asema BWANA. 9 Kum 28:12 Nami nimewapiga kwa ukame na kuvu; wingi wa bustani zenu na mashamba yenu ya mizabibu, na mitini yenu na mizeituni yenu imeliwa na tunutu; Lakini hamkunirudia mimi, asema BWANA. 10 Nimewaletea tauni, kama tauni ya Misri; vijana wenu nimewaua kwa upanga, na farasi wenu nimewachukulia mbali; nami nimeupandisha uvundo wa kambi zenu na kuuingiza katika mianzi ya pua zenu; lakini hamkunirudia mimi, asema BWANA. 11 Isa 13:19;Zek 3:2;Mwa 19:24 Baadhi yenu nimewaangamiza, kama hapo Mungu alipoiangamiza Sodoma na Gomora, nanyi mkawa kama kinga kilichonyakuliwa motoni; lakini hamkunirudia mimi, asema BWANA. 12 Eze 13:5;Mt 5:25,26;1 The 5:2;Ufu 3:3 Basi nitakutenda hivi, Ee Israeli, na kwa sababu nitakutenda hivi, ujiweke tayari kuonana na Mungu wako, Ee Israeli. 13 Zab 139:2;Dan 2:28;Mt 9:4;Yn 2:25;Kum 32:13;Isa 47:4 Kwa maana, angalia, yeye aifanyaye milima, na kuumba upepo, na kumwambia mwanadamu mawazo yake, afanyaye asubuhi kuwa giza, na kupakanyaga mahali pa dunia palipoinuka; BWANA, Mungu wa majeshi, ndilo jina lake.