1 Kwa kuwa watu wengi wameweza kuandika kwa utaratibu habari za mambo yaliyotimizwa katikati yetu, 2 Yn 15:27 kama walivyotuhadithia wale waliokuwa mashahidi wenye kuyaona, na watumishi wa lile neno tokea mwanzo, 3 Mdo 1:1 nimeona vema mimi nami, kwa kuwa nimejitafutia usahihi wa mambo hayo yote tangu mwanzo, kukuandikia kwa taratibu, Theofilo mtukufu, 4 upate kujua hakika ya mambo yale uliyofundishwa.
5 1 Nya 24:10 Zamani za Herode, mfalme wa Yudea, palikuwa na kuhani mmoja, jina lake Zakaria, wa kikundi cha ukuhani cha Abiya, na mkewe alikuwa mmojawapo wa uzao wa Haruni, jina lake Elisabeti. 6 Na wote wawili walikuwa wenye haki mbele za Mungu, wakiishi katika amri zote za Bwana na maagizo yake bila lawama. 7 Nao walikuwa hawana mtoto, maana Elisabeti alikuwa tasa, na wote wawili ni wazee sana.
8 Basi ikawa, alipokuwa akifanya kazi ya ukuhani wakati wa zamu yake mbele za Mungu, 9 Kut 30:7 kama ilivyokuwa desturi ya ukuhani, kura ilimwangukia kuingia katika hekalu la Bwana ili kufukiza uvumba. 10 Na makutano yote ya watu walikuwa wakisali nje saa ya kufukiza uvumba. 11 Akatokewa na malaika wa Bwana, amesimama upande wa kulia wa madhabahu ya kufukizia. 12 Zakaria alipomwona alifadhaika, hofu ikamwingia. 13 Lakini yule malaika akamwambia, Usiogope, Zakaria, maana dua yako imesikiwa, na mkeo Elisabeti atakuzalia mtoto wa kiume, na jina lake utamwita Yohana. 14 Nawe utakuwa na furaha na shangwe, na watu wengi watakufurahia kuzaliwa kwake. 15 Hes 6:3;Amu 13:4,5;1 Sam 1:11 Kwa sababu atakuwa mkuu mbele za Bwana; hatakunywa divai wala kileo; naye atajazwa Roho Mtakatifu hata tangu tumboni mwa mamaye. 16 Na wengi katika Waisraeli atawarejesha kwa Bwana Mungu wao. 17 Mal 3:1;4:5-6;Mt 17:11-13 Naye atatangulia mbele zake katika roho ya Eliya, na nguvu zake, ili kuigeuza mioyo ya baba iwaelekee watoto, na kuwatilia waasi akili za wenye haki, na kumwekea Bwana tayari watu waliotayarishwa. 18 Mwa 18:11 Zakaria akamwambia malaika, Nitajuaje neno hilo? Maana mimi ni mzee, na mke wangu ni mkongwe wa siku nyingi. 19 Dan 8:16;9:21;Ebr 1:14 Malaika akamjibu akamwambia, Mimi ni Gabrieli, nisimamaye mbele za Mungu; nami nimetumwa niseme nawe, na kukupasha habari hizi njema. 20 Lk 1:45 Na tazama! Utakuwa bubu, usiweze kusema, mpaka siku ile yatakapotukia hayo, kwa sababu hukuyasadiki maneno yangu; nayo yatatimizwa kwa wakati wake.
21 Na wale watu walikuwa wakimngojea Zakaria, wakastaajabia kukawia kwake mle hekaluni. 22 Alipotoka akiwa hawezi kusema nao, walitambua ya kuwa ameona maono ndani ya hekalu, naye aliendelea kuwaashiria akakaa bubu. 23 Ikawa siku za huduma yake zilipokuwa zimetimia akaenda nyumbani kwake. 24 Hata baada ya siku zile mkewe Elisabeti alichukua mimba akatawa miezi mitano, akisema, 25 Mwa 30:23 Hivi ndivyo alivyonitendea Bwana katika siku zile alizoniangalia ili kuniondolea aibu yangu mbele ya watu.
26 Mwezi wa sita, malaika Gabrieli alitumwa na Mungu kwenda mpaka katika mji wa Galilaya, jina lake Nazareti, 27 Mt 1:16,18;Lk 2:5 kwa mwanamwali bikira aliyekuwa ameposwa na mtu, jina lake Yusufu, wa ukoo wa Daudi; na jina lake bikira huyo ni Mariamu. 28 Amu 5:24 Akaingia nyumbani kwake akasema, Salamu, uliyepewa neema, Bwana yu pamoja nawe. 29 Naye akafadhaika sana kwa ajili ya maneno yake, akawaza moyoni, Salamu hii ni ya namna gani? 30 Malaika akamwambia, Usiogope, Mariamu, kwa maana umepata neema kwa Mungu. 31 Mt 1:21-23;Amu 13:3;Isa 7:14 Tazama, utachukua mimba na kuzaa mtoto wa kiume; na jina lake utamwita Yesu. 32 2 Sam 7:12,13,16;Isa 9:7 Huyo atakuwa mkuu, ataitwa Mwana wa Aliye Juu, na Bwana Mungu atampa kiti cha enzi cha Daudi, baba yake. 33 Mik 4:7;Dan 7:14 Ataimiliki nyumba ya Yakobo hata milele, na ufalme wake utakuwa hauna mwisho. 34 Mariamu akamwambia malaika, Litakuwaje neno hili, maana sijui mume? 35 Kut 13:12;Mt 1:18,20 Malaika akajibu akamwambia, Roho Mtakatifu atakujia juu yako, na nguvu zake Aliye Juu zitakufunika kama kivuli; kwa sababu hiyo hicho kitakachozaliwa kitaitwa kitakatifu, Mwana wa Mungu. 36 Tena, tazama, jamaa yako Elisabeti naye amechukua mimba ya mtoto wa kiume katika uzee wake; na mwezi huu ni wa sita kwake yeye aliyeitwa tasa; 37 Mwa 18:14 kwa kuwa hakuna neno lisilowezekana kwa Mungu. 38 Mariamu akasema, Tazama, mimi ni mjakazi wa Bwana; na iwe kwangu kama ulivyosema. Kisha malaika akaondoka akaenda zake.
39 Basi, Mariamu akaondoka siku hizo, akaenda hadi katika nchi yenye milima kwa haraka mpaka mji mmoja wa Yudea, 40 akaingia nyumbani kwa Zakaria akamwamkia Elisabeti. 41 Lk 1:15;Mwa 25:22 Ikawa Elisabeti aliposikia kule kuamkia kwake Mariamu, kitoto kichanga kikaruka ndani ya tumbo lake; Elisabeti akajazwa Roho Mtakatifu; 42 Kum 28:9;Amu 5:24 akapaza sauti kwa nguvu akasema, Umebarikiwa wewe katika wanawake, naye mzao wa tumbo lako amebarikiwa. 43 Limenitokeaje neno hili, hata mama wa Bwana wangu anijie mimi? 44 Maana sauti ya kuamkia kwako ilipoingia masikioni mwangu, kitoto kichanga kikaruka kwa shangwe ndani ya tumbo langu. 45 Lk 1:20;11:28 Naye heri aliyesadiki; kwa maana yatatimizwa aliyoambiwa na Bwana.
46 1 Sam 2:1-10 Mariamu akasema,
Moyo wangu wamwadhimisha Bwana,
47 Na roho yangu imemfurahia Mungu, Mwokozi wangu;
48 1 Sam 1:11;Lk 1:25;Zab 113:5,6;Lk 11:27 Kwa kuwa ameutazama
Unyonge wa mjakazi wake.
Kwa maana, tazama, tokea sasa
Vizazi vyote wataniita mbarikiwa;
49 Zab 111:9 Kwa kuwa Mwenye nguvu amenitendea makuu,
Na jina lake ni takatifu.
50 Zab 103:13,17 Na rehema zake hudumu vizazi hata vizazi
Kwa hao wanaomcha.
51 Zab 89:10;2 Sam 22:28 Amefanya nguvu kwa mkono wake;
Amewatawanya walio na kiburi katika mawazo ya mioyo yao;
52 Ayu 5:11;12:19;Zab 147:6;1 Sam 2:7 Amewaangusha wakuu katika viti vyao vya enzi;
Na wanyonge amewainua.
53 1 Sam 2:5;Zab 34:10;107:9 Wenye njaa amewashibisha mema,
Na wenye mali amewaondoa mikono mitupu.
54 Isa 41:8;Zab 98:3 Amemsaidia Israeli, mtumishi wake;
Ili kukumbuka rehema zake;
55 Mwa 17:7;18:18;22:17;Mik 7:20 Kama alivyowaambia baba zetu,
Abrahamu na uzao wake hata milele.
56 Mariamu akakaa naye kadiri ya miezi mitatu, kisha akarudi kwenda nyumbani kwake.
57 Ikawa, siku za kuzaa kwake Elisabeti zilipotimia, alizaa mtoto mwanamume. 58 Wakasikia jirani zake na jamaa zake ya kwamba Bwana amemwongezea rehema zake, wakafurahi pamoja naye. 59 Law 12:3;Mwa 17:12 Ikawa siku ya nane wakaja kumtahiri mtoto; wakataka kumpa jina la babaye, Zakaria. 60 Lk 1:13 Mamaye akajibu akasema La, sivyo; bali, ataitwa Yohana. 61 Wakamwambia, Hapana mtu katika jamaa zako aitwaye jina hilo. 62 Wakamwashiria babaye wajue atakavyo kumwita. 63 Akataka kibao, akaandika ya kwamba, Jina lake ni Yohana. Wakastaajabu wote. 64 Papo hapo kinywa chake kikafunguliwa na ulimi wake pia, akaanza kunena akimsifu Mungu. 65 Wakaingiwa na hofu wote waliokuwa wakikaa karibu nao; na mambo hayo yote yakatangazwa katika nchi yote ya Yudea yenye milima. 66 Na wote walioyasikia wakayaweka mioyoni mwao, wakisema, Mtoto huyu atakuwa wa namna gani? Kwa sababu mkono wa Bwana ulikuwa pamoja naye.
67 Na Zakaria, baba yake, akajazwa Roho Mtakatifu, akatabiri, akisema,
68 Lk 7:16;Zab 41:13;72:18 Atukuzwe Bwana, Mungu wa Israeli,
Kwa kuwa amewajia watu wake, na kuwakomboa.
69 1 Sam 2:10;Zab 18:2;132:17 Ametusimamishia pembe ya wokovu
Katika mlango wa Daudi, mtumishi wake.
70 Kama alivyosema tangu mwanzo
Kwa kinywa cha manabii wake watakatifu;
71 Zab 106:10 Tuokolewe na adui zetu
Na mikononi mwao wote wanaotuchukia;
72 Zab 105:8;106:45;Mwa 17:7;Law 26:42 Ili kuwatendea rehema baba zetu,
Na kulikumbuka agano lake takatifu;
73 Mwa 22:16,17;Mik 7:20 Kiapo alichomwapia Abrahamu, baba yetu,
74 Tit 2:12,14 Ya kwamba atatujalia sisi,
Tuokoke mikononi mwa adui zetu,
Na kumwabudu pasipo hofu,
75 Kwa utakatifu na kwa haki
Mbele zake siku zetu zote.
76 Mal 3:1;Mt 3:3 Nawe, mtoto, utaitwa nabii wake Aliye Juu,
Kwa maana utatangulia mbele za uso wa Bwana umtengenezee njia zake;
77 Yer 31:34 Uwajulishe watu wake wokovu,
Kwa kusamehewa dhambi zao.
78 Hes 24:17;Isa 60:1,2;Mal 4:2 Kwa njia ya rehema za Mungu wetu,
Ambazo kwa hizo mwangaza utokao juu umetufikia,
79 Isa 9:2;58:8;Mt 4:16 Kuwaangaza wakaao katika giza na uvuli wa mauti,
Na kuiongoza miguu yetu kwenye njia ya amani.
80 Mt 3:1 Yule mtoto akakua, akaongezeka nguvu rohoni, akakaa majangwani hadi siku ile alipotokeza hadharani kwa Israeli.