1 Mt 24:1-51;Lk 21:5-36 Alipokuwa akitoka hekaluni, mmoja wa wanafunzi wake alimwambia, Mwalimu, tazama, yalivyo mawe na majengo haya! 2 Yesu akajibu, akamwambia, Wayaona majengo haya makubwa? Halitabaki hapa jiwe juu ya jiwe ambalo halitabomolewa.
3 Na alipokuwa ameketi katika mlima wa Mizeituni, kuelekea hekalu Petro, na Yakobo, na Yohana, na Andrea walimwuliza kwa faragha, 4 Tuambie, mambo hayo yatakuwa lini? Nayo ni nini dalili ya wakati, hayo yote yatakapokuwa karibu kutimia?
5 Yesu akaanza kuwaambia, Jihadharini, mtu asiwadanganye. 6 Wengi watakuja kwa jina langu, wakisema, Mimi ndiye, nao watadanganya wengi. 7 Nanyi mtakaposikia habari za vita na uvumi wa vita, msitishwe; hayo hayana budi kutukia, lakini ule mwisho bado. 8 Isa 19:2;2 Nya 15:6 Kwa maana taifa litaondoka kupigana na taifa, na ufalme kupigana na ufalme; kutakuwa na mitetemeko ya ardhi mahali kwingi; kutakuwako na njaa; hayo ndiyo mwanzo wa uchungu.
9 Mt 10:17-20;Lk 12:11-12 Nanyi jihadharini nafsi zenu; maana watawapeleka ninyi mabarazani; na katika masinagogi mtapigwa; nanyi mtachukuliwa mbele ya watawala na wafalme kwa ajili yangu, kuwa ushuhuda kwao. 10 Mk 16:15 Na sharti Injili ihubiriwe kwanza katika mataifa yote. 11 Na watakapowachukua ninyi, na kuwasaliti, msitafakari kwanza mtakayosema, lakini lolote mtakalopewa saa ile, lisemeni; kwa maana si ninyi msemao, bali ni Roho Mtakatifu. 12 Mik 7:6 Na ndugu atamsaliti ndugu yake ili auawe, na baba atamsaliti mtoto, na watoto watashambulia wazazi wao, na kuwaua. 13 Mt 10:22;Yn 15:21 Nanyi mtakuwa mkichukiwa na watu wote kwa ajili ya jina langu; lakini mwenye kuvumilia hadi mwisho, ndiye atakayeokoka.
14 Dan 9:27;11:31;12:11 Lakini mlionapo chukizo la uharibifu likisimama pasipolipasa, (asomaye na afahamu), ndipo walio katika Yudea na wakimbilie milimani; 15 Lk 17:31 na mtu aliye juu ya dari asishuke, wala asiingie kuchukua kitu nyumbani mwake; 16 naye aliye shambani asirudi nyuma kulichukua vazi lake. 17 Lakini ole wao wenye mimba, nao wanyonyeshao siku hizo! 18 Ila ombeni yasitokee hayo wakati wa baridi. 19 Dan 12:1;Mdo 7:14;Yoe 2:2 Kwa maana siku hizo zitakuwa na dhiki, jinsi isivyokuwa tangu mwanzo wa kuumba alipoumba Mungu hata sasa, wala haitakuwa kamwe. 20 Na kama Bwana asingalizikatiza siku hizo, asingeokoka mtu yeyote; lakini kwa ajili ya wateule aliowateua amezikatiza siku hizo. 21 Na wakati huo mtu akiwaambia, Tazama, Kristo yupo hapa, au yuko kule, msisadiki; 22 Kum 13:1 kwa maana watajitokeza Makristo wa uongo, na manabii wa uongo, watatoa ishara na maajabu, wapate kuwadanganya, ikiwezekana, hata hao wateule. 23 Bali ninyi jihadharini; nimekwisha kuwaonya yote mbele.
24 Isa 13:10;Eze 32:7;Yoe 2:10,31;3:15;Ufu 6:12 Lakini siku zile, baada ya dhiki hiyo, jua litatiwa giza, na mwezi hatautoa mwanga wake. 25 Isa 34:4;Yoe 2:10;Mdo 6:13 Na nyota za mbinguni zitakuwa zikianguka, na nguvu zilizo mbinguni zitatikisika. 26 Dan 7:13;Ufu 1:7 Hapo ndipo watakapomwona Mwana wa Adamu akija mawinguni kwa nguvu nyingi na utukufu. 27 Zek 2:6;Kum 30:4;Mt 13:41 Ndipo atakapowatuma malaika na kuwakusanya wateule wake toka pepo nne, toka upande wa mwisho wa nchi hata upande wa mwisho wa mbingu.
28 Kwa mtini jifunzeni mfano; tawi lake liishapo kuwa laini, na kuchanua majani, mwatambua ya kuwa wakati wa mavuno ni karibu; 29 nanyi kadhalika, myaonapo mambo hayo yanaanza, tambueni ya kuwa yu karibu milangoni. 30 Amin, nawaambieni, Kizazi hiki hakitapita, hata hayo yote yatimie. 31 Mbingu na nchi zitapita; lakini maneno yangu hayatapita kamwe.
32 Mt 24:36 Lakini habari ya siku ile na saa ile hakuna aijuaye, hata malaika walio mbinguni, wala Mwana, ila Baba.
33 Angalieni, kesheni, [ombeni], kwa kuwa hamjui wakati ule utakapokuwapo. 34 Lk 12:36-38;19:12;Mt 25:14 Mfano wake ni kama mtu mwenye kusafiri, ameiacha nyumba yake, amewapa watumwa wake amri, na kila mtu kazi yake, naye amemwamuru bawabu akeshe. 35 Lk 12:38 Kesheni basi, kwa maana hamjui ajapo bwana wa nyumba, kwamba ni jioni, au kwamba ni usiku wa manane, au awikapo jogoo, au asubuhi; 36 asije akawasili ghafla akawakuta mmelala. 37 Na hilo niwaambialo ninyi, nawaambia wote, Kesheni.