15 Hata kulipokuwa jioni, wanafunzi wake walimwendea, wakasema, Mahali hapa ni nyika tupu, na saa imekwisha pita; uwaage makutano, waende zao vijijini, wakajinunulie vyakula. 16 Yesu akawaambia, Hawana haja kwenda zao, wapeni ninyi vyakula. 17 Wakamwambia, Hamna kitu hapa ila mikate mitano na samaki wawili. 18 Akasema, Nileteeni hapa. 19 Akawaagiza makutano waketi katika majani; akaitwaa ile mikate mitano na wale samaki wawili, akatazama juu mbinguni, akabariki, akaimega ile mikate, akawapa wanafunzi, wanafunzi wakawapa makutano. 20 2 Fal 4:44Wakala wote wakashiba; wakayaokota mabaki ya vipande vya mikate, vikapu kumi na viwili, vimejaa. 21 Nao waliokula walikuwa wanaume wapatao elfu tano, bila kuhesabu wanawake na watoto.