Wageni kutoka mashariki
1 Lk 2:1-7Yesu alipozaliwa katika Bethlehemu ya Uyahudi zamani za mfalme Herode, tazama, majusi wa mashariki walifika Yerusalemu, wakisema, 2 Hes 24:17Yuko wapi yeye aliyezaliwa mfalme wa Wayahudi? Kwa maana tuliiona nyota yake mashariki, nasi tumekuja kumsujudia. 3 Basi mfalme Herode aliposikia hayo, alifadhaika, na Yerusalemu pia pamoja naye. 4 Akakusanya wakuu wa makuhani wote na waandishi wa watu, akatafuta habari kwao, Kristo azaliwa wapi? 5 Mik 5:2;Yn 7:42Nao wakamwambia, Katika Bethlehemu ya Yudea; kwa maana ndivyo ilivyoandikwa na nabii,
6 Mik 5:1Nawe Bethlehemu, katika nchi ya Yuda,
Hu mdogo kamwe miongoni mwa watawala wa Yuda;
Kwa kuwa kwako atatoka mtawala
Atakayewachunga watu wangu Israeli.
7 Kisha Herode akawaita wale majusi faraghani, akapata kwao hakika ya muda tangu ilipoonekana ile nyota. 8 Akawatuma Bethlehemu, akasema, Nendeni mkachunguze kwa makini habari za mtoto; na mkiisha kumwona, nileteeni habari, ili mimi nami niende nimsujudie. 9 Nao waliposikia maneno ya mfalme, walishika njia; na tazama, ile nyota waliyoiona mashariki ikawatangulia, mpaka iliposimama juu ya mahali alipokuwapo mtoto. 10 Nao walipoiona ile nyota, walifurahi furaha kubwa mno. 11 Zab 72:10,15;Isa 60:6Wakaingia nyumbani, wakamwona mtoto pamoja na Mariamu mamaye, wakaanguka wakamsujudia; nao walipokwisha kufungua hazina zao, wakamtolea tunu; dhahabu, uvumba na manemane. 12 Nao wakiisha kuonywa na Mungu katika ndoto wasimrudie Herode, wakaenda zao kwao kwa njia nyingine.