1 Rum 7:23;1 Pet 2:11 Vita vyatoka wapi, na mapigano yaliyoko kati yenu yatoka wapi? Si humu, katika tamaa zenu zifanyazo vita katika viungo vyenu? 2 Mwatamani, wala hamna kitu, mwaua na kuona wivu, wala hamwezi kupata. Mwafanya vita na kupigana, wala hamna kitu kwa kuwa hamwombi! 3 Hata mwaomba, wala hampati kwa sababu mwaomba vibaya, ili mvitumie kwa tamaa zenu. 4 Lk 6:26;Rum 8:7;1 Yoh 2:15 Enyi wazinzi, hamjui ya kwamba kuwa rafiki wa dunia ni kuwa adui wa Mungu? Basi kila atakaye kuwa rafiki wa dunia hujifanya kuwa adui wa Mungu. 5 Kut 20:3,5;Mt 6:24;Gal 5:17 Au mwadhani ya kwamba Maandiko yasema bure? Huyo Roho akaaye ndani yetu hututamani kiasi cha kuona wivu? 6 Mit 3:34;Ayu 22:29;Mt 23:12;1 Pet 5:5 Lakini hutujalia sisi neema iliyozidi; kwa hiyo husema, Mungu huwapinga wajikuzao, bali huwapa neema wanyenyekevu. 7 Efe 6:12;1 Pet 5:8,9 Basi mtiini Mungu. Mpingeni Shetani, naye atawakimbia. 8 Zek 1:3;Isa 1:16 Mkaribieni Mungu, naye atawakaribia ninyi. Itakaseni mikono yenu, enyi wenye dhambi, na kuisafisha mioyo yenu, enyi wenye nia mbili. 9 Huzunikeni na kuomboleza na kulia. Kucheka kwenu na kugeuzwe kuwa kuomboleza, na furaha yenu kuwa huzuni kubwa. 10 1 Pet 5:6 Jidhilini mbele za Bwana, naye atawakuza.
11 Ndugu, msisingiziane; amsingiziaye ndugu yake, au kumhukumu ndugu yake, huisingizia sheria na kuihukumu sheria. Lakini ukiihukumu sheria, huwi mtenda sheria, bali umekuwa hakimu. 12 Mk 7:1;Rum 2:1;14:4 Mtoa sheria na mwenye kuhukumu ni mmoja tu, ndiye awezaye kuokoa na kuangamiza. U nani wewe umhukumuye mtu mwingine?
13 Mit 27:1 Haya basi, ninyi msemao, Leo au kesho tutaingia katika mji fulani na kukaa humo mwaka mzima, na kufanya biashara na kupata faida; 14 Lk 12:20;Zab 39:5,11 lakini hamjui yatakayokuwako kesho. Uzima wenu ni nini? Maana ninyi ni mvuke uonekanao kwa muda mfupi tu, kisha hutoweka. 15 Mdo 18:21 Badala ya kusema, Bwana akipenda, tutakuwa hai na kufanya hivi au hivi. 16 Lakini sasa mwajisifu katika majivuno yenu; kujisifu kote kwa namna hii ni kubaya. 17 Lk 12:47;Rum 14:23 Basi yeye ajuaye kutenda mema, wala hayatendi, kwake huyo ni dhambi.