25 Wakati huo huko Yerusalemu kulikuwa na mtu mmoja, mwema na mcha Mungu, jina lake Simeoni. Yeye alikuwa akitazamia kwa hamu ukombozi wa Israeli. Roho Mtakatifu alikuwa pamoja naye.
26 Roho Mtakatifu alikuwa amemhakikishia kwamba hatakufa kabla ya kumwona Masiha wa Bwana.
27 Basi, akiongozwa na Roho Mtakatifu, Simeoni aliingia Hekaluni; na wazazi wa Yesu walipomleta Hekaluni mtoto wao ili wamfanyie kama ilivyotakiwa na Sheria,
28 Simeoni alimpokea mtoto Yesu mikononi mwake huku akimtukuza Mungu na kusema:
29 "Sasa Bwana, umetimiza ahadi yako, waweza kumruhusu mtumishi wako aende kwa amani.
30 Maana kwa macho yangu nimeuona wokovu utokao kwako,
31 ambao umeutayarisha mbele ya watu wote:
32 Mwanga utakaowaangazia watu wa mataifa, na utukufu kwa watu wako Israeli."