54 Basi, wakamkamata, wakamchukua na kwenda naye nyumbani kwa Kuhani Mkuu. Petro akawa anamfuata nyuma kwa mbali.

55 Moto ulikuwa umewashwa katikati ya ua, nao wakawa wameketi pamoja Petro akiwa miongoni mwao.

56 Mjakazi mmoja alipomwona Petro ameketi karibu na moto, akamkodolea macho, akasema, "Mtu huyu alikuwa pia pamoja na Yesu."

57 Lakini Petro akakana akisema, "Wee! simjui mimi."

58 Baadaye kidogo, mtu mwingine akamwona Petro, akasema, "Wewe ni mmoja wao." Lakini Petro akajibu "Bwana we; si mimi!"

59 Kama saa moja baadaye, mtu mwingine akasisitiza, "Hakika huyu alikuwa pamoja naye; ametoka Galilaya ati."

60 Lakini Petro akasema, "Bwana wee; sijui hata unachosema!" Na papo hapo, akiwa bado anaongea, jogoo akawika.

61 Bwana akageuka na kumtazama Petro, naye Petro akakumbuka yale aliyokuwa ameambiwa na Bwana: "Leo kabla jogoo hajawika, utanikana mara tatu."

62 Hapo akatoka nje, akalia sana.