23 Ole wenu walimu wa Sheria na Mafarisayo, wanafiki! Mnatoza watu zaka, hata juu ya majani yenye harufu nzuri, bizari na jira, na huku mnaacha mambo muhimu ya Sheria kama vile haki, huruma na imani. Haya ndiyo hasa mliyopaswa kuyazingatia bila kusahau yale mengine.
24 Viongozi vipofu! Mnatoa nzi katika kinywaji, lakini mnameza ngamia! ic
25 "Ole wenu walimu wa Sheria na Mafarisayo, wanafiki! Mnasafisha kikombe na bakuli kwa nje, lakini ndani mnaacha kumejaa vitu mlivyopata kwa unyanganyi na uchoyo.
26 Mfarisayo kipofu! Kisafishe kikombe ndani kwanza na nje kutakuwa safi pia.
27 "Ole wenu walimu wa Sheria na Mafarisayo, wanafiki! Mko kama makaburi yaliyopakwa chokaa ambayo kwa nje yanaonekana kuwa mazuri, lakini ndani yamejaa mifupa ya maiti na kila namna ya uchafu.
28 Hali kadhalika ninyi mnaonekana na watu kwa nje kuwa wema, lakini kwa ndani mmejaa unafiki na uovu.
29 "Ole wenu walimu wa Sheria na Mafarisayo, wanafiki! Mnajenga makaburi ya manabii na kuyapamba makaburi ya watu wema.
30 Mwasema: Kama sisi tungaliishi nyakati za wazee wetu hatungalishirikiana nao katika mauaji ya manabii!
31 Hivyo mnathibitisha ninyi wenyewe kwamba ninyi ni watoto wa watu waliowaua manabii.
32 Haya, kamilisheni ile kazi wazee wenu waliyoianza!
33 Enyi kizazi cha nyoka wenye sumu! Mnawezaje kuiepa hukumu ya moto wa Jehanamu?