1 Siku hizo Yohane Mbatizaji alitokea, akaanza kuhubiri katika jangwa la Yudea:

2 "Tubuni, maana Ufalme wa mbinguni umekaribia."

3 Huyu Yohane ndiye yule ambaye nabii Isaya alinena juu yake aliposema: "Sauti ya mtu imesikika jangwani: Mtayarishieni Bwana njia yake, nyoosheni vijia vyake."

4 Yohane alivaa vazi lililoshonwa kwa manyoya ya ngamia, na ukanda wa ngozi kiunoni mwake. Chakula chake kilikuwa nzige na asali ya mwituni.

5 Basi, watu kutoka Yerusalemu, kutoka mkoa wote wa Yudea na sehemu zote za kandokando ya mto Yordani, walimwendea,

6 wakaziungama dhambi zao, naye akawabatiza katika mto Yordani.