Arca da aliança
A Arca da Aliança era o símbolo mais sagrado de Israel — representava a presença de Deus no meio do seu povo. Sobre ela brilhava a glória do Senhor entre os querubins.
"Nao watatengeneza Sanduku la mbao za mshita, lenye urefu wa dhiraa mbili na nusu, upana wa dhiraa moja na nusu, na kimo cha dhiraa moja na nusu. Utalifunika hilo Sanduku kwa dhahabu safi ndani na nje, na kulifanyia ukingo wa dhahabu juu yake kulizunguka. Utalisubu kwa pete nne za dhahabu na kuzifungia kwenye miguu yake minne, pete mbili kwa upande mmoja na pete mbili kwa upande mwingine. Kisha utatengeneza mipiko ya mti wa mshita na kuzifunika kwa dhahabu. Utaiingiza hiyo mipiko kwenye zile pete katika pande mbili za Sanduku ili kulibeba. Hiyo mipiko itabakia daima katika hizo pete za hilo Sanduku; haitaondolewa. Kisha weka ndani ya hilo Sanduku ule Ushuhuda nitakaokupa.
"Tengeneza kifuniko cha upatanisho cha dhahabu safi, chenye urefu wa dhiraa mbili na nusu, na upana wa dhiraa moja na nusu. Tengeneza makerubi wawili wa dhahabu iliyofuliwa katika miisho ya hicho kifuniko. Tengeneza kerubi mmoja kwenye mwisho mmoja, na kerubi mwingine kwenye mwisho mwingine; watengeneze makerubi hao wawe kitu kimoja na hicho kifuniko katika miisho hiyo miwili. Makerubi hao watakuwa wametandaza mabawa kuelekea juu, wakitia kivuli hicho kifuniko. Makerubi hao wataelekeana, wakitazama hicho kifuniko. Weka huo Ushuhuda nitakaokupa ndani ya hilo Sanduku la Agano, na uweke hicho kifuniko juu ya hilo Sanduku.
Hapo juu ya hicho kifuniko, kati ya hao makerubi wawili walio juu ya hilo Sanduku la Ushuhuda, hapo ndipo nitakutana nawe na kukupa maagizo yangu kwa ajili ya Waisraeli.
Bezaleli akatengeneza Sanduku la mbao za mshita: urefu wake ulikuwa dhiraa mbili na nusu, upana wake dhiraa moja na nusu, na kimo chake dhiraa moja na nusu.
Kisha Mwenyezi Mungu akamwambia Musa: "Simika maskani ya Mungu, lile Hema la Kukutania, katika siku ya kwanza ya mwezi wa kwanza. Weka Sanduku la Ushuhuda ndani yake na ulifunike kwa pazia. Ingiza meza na kupanga vitu vyake juu yake.
Akachukua ule Ushuhuda na kuuweka ndani ya Sanduku la Agano, akaweka ile mipiko ya kubebea hilo Sanduku na kuweka kiti cha rehema juu yake. Kisha Musa akalileta Sanduku ndani ya maskani ya Mungu, akatundika pazia ili kulifunika Sanduku la Ushuhuda, kama Mwenyezi Mungu alivyomwagiza.
Musa alipoingia kwenye Hema la Kukutania kuzungumza na Mwenyezi Mungu, alisikia sauti ikisema naye kutoka kati ya wale makerubi wawili waliokuwa juu ya kile kiti cha rehema, juu ya Sanduku la Ushuhuda. Musa akazungumza na Mwenyezi Mungu.
Hivyo waliondoka kutoka mlima wa Mwenyezi Mungu, nao wakasafiri kwa siku tatu. Sanduku la Agano la Mwenyezi Mungu liliwatangulia kwa zile siku tatu ili kuwatafutia mahali pa kupumzika. Wingu la Mwenyezi Mungu lilikuwa juu yao wakati wa mchana walipoondoka kambini.
Wakati wowote Sanduku lilipoondoka, Musa alisema,
"Ee Mwenyezi Mungu, inuka!
Watesi wako na watawanyike;
adui zako na wakimbie mbele zako."
Wakati wowote Sanduku liliposimama, alisema,
"Ee Mwenyezi Mungu, rudi,
kwa maelfu ya Waisraeli wasiohesabika."
Mwenyezi Mungu akamwambia Musa, "Sema na Waisraeli, na ujipatie fimbo kumi na mbili kutoka kwao, moja kutoka kwa kila mmoja wa viongozi wa makabila ya baba zao. Andika jina la kila mtu kwenye fimbo yake. Kwenye fimbo ya Lawi andika jina la Haruni, kwa maana ni lazima iwepo fimbo moja kwa kila kiongozi kwa ajili ya kila kabila la baba zao. Ziweke hizo fimbo ndani ya Hema la Kukutania mbele ya Sanduku la Ushuhuda, mahali nikutanapo nawe. Fimbo ya mtu nitakayemchagua itachipuka, nami mwenyewe nitayakomesha haya manung’uniko ya mara kwa mara ya Waisraeli dhidi yako."
Hivyo Musa akasema na Waisraeli, nao viongozi wao wakampa fimbo kumi na mbili, fimbo moja kwa ajili ya kila kabila la baba zao, nayo fimbo ya Haruni ikiwa miongoni mwa hizo. Musa akaziweka hizo fimbo mbele za Mwenyezi Mungu ndani ya Hema la Ushuhuda.
Siku iliyofuata Musa aliingia kwenye Hema la Ushuhuda akaona ile fimbo ya Haruni ambayo iliwakilisha jamaa ya Lawi haikuwa tu imechipuka, bali pia ilikuwa imetoa machipukizi, kuchanua maua na kuzaa malozi. Ndipo Musa akaleta zile fimbo zote kwa Waisraeli wote kutoka mbele za Mwenyezi Mungu. Wakaziangalia, na kila mtu akaichukua fimbo yake mwenyewe.
Mwenyezi Mungu akamwambia Musa, "Rudisha fimbo ya Haruni mbele ya Sanduku la Ushuhuda, ili ihifadhiwe kama alama kwa waasi. Hili litakomesha manung’uniko yao dhidi yangu, ili wasife." Musa akafanya kama Mwenyezi Mungu alivyomwamuru.
Basi, watu walipovunja kambi ili kuvuka Yordani, makuhani wakiwa wamebeba Sanduku la Agano waliwatangulia. Wakati huu ulikuwa wakati wa mavuno, nao Mto Yordani ulikuwa umefurika hadi kwenye kingo zake. Ilikuwa kawaida ya Yordani kufurika nyakati zote za mavuno. Mara tu makuhani wale waliokuwa wamebeba Sanduku la Agano walipofika mtoni na nyayo zao kuzama ndani ya yale maji, maji hayo yaliyotiririka kutoka upande wa juu yaliacha kutiririka yakasimama kama chuguu mbali kabisa nao, kwenye mji ulioitwa Adamu kwenye eneo la Sarethani, wakati yale maji yaliyokuwa yanatiririka kuingia kwenye Bahari ya Araba (yaani Bahari ya Chumvi), yalitindika kabisa. Hivyo watu wakavuka kukabili Yeriko.
Wale makuhani waliobeba Sanduku la Agano la Mwenyezi Mungu, wakasimama imara mahali pakavu katikati ya Mto Yordani, wakati Waisraeli wote wakiwa wanapita hadi taifa lote likaisha kuvuka mahali pakavu.
Nao makuhani wakapanda kutoka ndani ya Mto Yordani wakilibeba hilo Sanduku la Agano la Mwenyezi Mungu. Mara tu walipoiweka miguu yao ukingoni mwa mto, maji ya Yordani yakarudi kufurika kama ilivyokuwa kabla.
Basi malango ya Yeriko yalifungwa kwa uthabiti kwa sababu ya Waisraeli. Hakuna mtu yeyote aliyetoka au kuingia.
Kisha Mwenyezi Mungu akamwambia Yoshua, "Tazama, nimeitia Yeriko mikononi mwako, pamoja na mfalme wake na wapiganaji wake. Zunguka mji mara moja pamoja na watu wote wenye silaha. Fanya hivi kwa siku sita. Uwe na makuhani saba wakibeba mabaragumu ya pembe za kondoo dume mbele ya Sanduku. Siku ya saba, mzunguke mji mara saba, nao makuhani wakipiga baragumu hizo. Utakapowasikia wamepaliza sauti kubwa ya baragumu, watu wote wapige kelele kwa sauti kuu, kisha ukuta wa mji utaanguka na wapiganaji watapanda, kila mtu akielekea mbele yake."
Ndipo Yoshua mwana wa Nuni akaita makuhani na kuwaambia, "Chukueni Sanduku la Agano la Mwenyezi Mungu na makuhani saba wachukue baragumu za pembe za kondoo dume mbele yake." Naye akawaagiza watu, "Songeni mbele! Mkauzunguke mji, na walinzi wenye silaha watangulie mbele ya Sanduku la Mwenyezi Mungu."
Baragumu zilipopigwa, watu walipiga kelele; kwa ile sauti ya baragumu na watu kupaza sauti, ukuta ukaanguka; hivyo kila mtu akapanda akiendelea mbele na kuuteka mji.
Wafilisti wakapanga safu za majeshi yao kupambana na Israeli, wakati vita vilipoenea, Israeli wakashindwa na Wafilisti, ambao waliwaua askari wa Israeli wapatao elfu nne kwenye uwanja wa vita. Askari waliporudi kambini, wazee wa Israeli wakawauliza, "Kwa nini Mwenyezi Mungu ameruhusu leo tushindwe mbele ya Wafilisti? Tuleteni Sanduku la Agano la Mwenyezi Mungu kutoka Shilo, ili lipate kwenda pamoja nasi, na kutuokoa kutoka mikono ya adui zetu."
Hivyo wakawatuma watu huko Shilo, nao wakalichukua Sanduku la Agano la Mwenyezi Mungu, Mungu wa majeshi ya mbinguni, aliyekaa kwenye kiti chake cha enzi kati ya makerubi. Nao Hofni na Finehasi, wale wana wawili wa Eli, walikuwa huko na Sanduku la Agano la Mungu.
Wakati Sanduku la Agano la Mwenyezi Mungu lilikuja kambini, Waisraeli wote wakapiga kelele kwa sauti kuu hata ardhi ikatikisika. Wafilisti waliposikia makelele, wakauliza, "Kwa nini kuna makelele haya yote katika kambi ya Waebrania?"
Walipofahamu kuwa Sanduku la Mwenyezi Mungu limekuja kambini, Wafilisti wakaogopa, wakasema, "Mungu amekuja kambini, ole wetu. Halijatokea jambo kama hili tangu hapo awali. Ole wetu! Ni nani atakayetuokoa kutoka mikononi mwa miungu hii yenye nguvu? Ni miungu ile iliyowapiga Wamisri kwa mapigo ya aina zote huko jangwani. Tuweni hodari, enyi Wafilisti! Tuweni wanaume, la sivyo mtakuwa watumwa wa Waebrania, kama wao walivyokuwa kwenu. Kuweni wanaume, mpigane!"
Basi Wafilisti wakapigana, nao Waisraeli wakashindwa na kila mtu akakimbilia kwenye hema lake. Mauaji yalikuwa makubwa sana, Israeli wakapoteza askari elfu thelathini walioenda kwa miguu. Sanduku la Mungu likatekwa, na hao wana wawili wa Eli, Hofni na Finehasi, wakauawa.
Mkono wa Mwenyezi Mungu ulikuwa mzito juu ya watu wa Ashdodi na vijiji jirani, akaleta uharibifu juu yao na kuwatesa kwa majipu. Watu wa Ashdodi walipoona kile kilichokuwa kikitokea, wakasema, "Sanduku la Mungu wa Israeli kamwe lisikae hapa pamoja na sisi, kwa sababu mkono wake ni mzito juu yetu na juu ya Dagoni mungu wetu." Basi wakawaita watawala wote wa Wafilisti pamoja na kuwauliza, "Tutafanya nini na hili Sanduku la Mungu wa Israeli?"
Wakajibu, "Sanduku la Mungu wa Israeli na liende Gathi." Basi wakalihamisha Sanduku la Mungu wa Israeli.
Lakini baada ya kulihamisha, mkono wa Mwenyezi Mungu ulikuwa dhidi ya huo mji wa Gathi, akiuweka katika fadhaa kuu. Mungu akawatesa watu wa huo mji, vijana kwa wazee, kwa kuwaletea majipu. Basi wakapeleka Sanduku la Mungu Ekroni.
Sanduku la Mungu lilipokuwa linaingia Ekroni, watu wa Ekroni walilia wakisema, "Wamelileta Sanduku la Mungu wa Israeli kwetu ili kutuua sisi na watu wetu." Basi wakawaita watawala wote wa Wafilisti pamoja na kusema, "Liondoeni Sanduku la Mungu wa Israeli na lirudishwe mahali pake, la sivyo litatuua sisi na watu wetu." Kwa kuwa kifo kilikuwa kimeujaza mji hofu; kwani mkono wa Mungu ulikuwa mzito sana juu yake.
Sanduku la Mwenyezi Mungu lilipokuwa limekaa katika nchi ya Wafilisti kwa miezi saba, Wafilisti waliwaita makuhani wa Dagoni na waaguzi, na kuwaambia, "Tutafanya nini na hili Sanduku la Mwenyezi Mungu? Tuambieni jinsi tutakavyolirudisha mahali pake."
Wakajibu, "Kama mtalirudisha Sanduku la Mungu wa Israeli, msilirudishe mikono mitupu bali kwa vyovyote mpelekeeni sadaka ya hatia. Kisha mtaponywa, nanyi mtafahamu kwa nini mkono wake haujaondolewa kwenu."
Basi wakafanya hivyo. Wakachukua ng’ombe wawili wa aina hiyo, wakawafungia hilo gari la kukokotwa, nao ndama wao wakawekwa zizini. Wakaliweka Sanduku la Mwenyezi Mungu juu ya hilo gari la kukokotwa pamoja na lile kasha lenye ile mifano ya panya wa dhahabu na ya majipu ya dhahabu. Kisha hao ng’ombe wakaenda moja kwa moja kuelekea Beth-Shemeshi, wakishuka bila kugeuka kuume au kushoto, huku wakilia njia yote. Watawala wa Wafilisti waliwafuata hao ng’ombe hadi mpakani mwa Beth-Shemeshi.
Wakati huu watu wa Beth-Shemeshi walikuwa wakivuna ngano yao huko bondeni, walipoinua macho yao na kuona lile Sanduku, wakafurahi kuliona. Lile gari la kukokotwa lilikuja kwenye shamba la Yoshua wa Beth-Shemeshi, nalo likasimama kando ya mwamba mkubwa. Watu wakapasua mbao za lile gari la kukokotwa na kutoa dhabihu wale ng’ombe kuwa sadaka ya kuteketezwa kwa Mwenyezi Mungu. Walawi walilishusha Sanduku la Mwenyezi Mungu, pamoja na lile kasha lililokuwa na vile vitu vya dhahabu na kuviweka juu ya ule mwamba mkubwa. Siku ile watu wa Beth-Shemeshi wakatoa sadaka za kuteketezwa na dhabihu kwa Mwenyezi Mungu.
Kisha wanaume wa Kiriath-Yearimu wakaja na kulichukua Sanduku la Mwenyezi Mungu. Wakalipeleka katika nyumba ya Abinadabu kilimani, na kumweka Eleazari mwanawe wakfu kulichunga Sanduku la Mwenyezi Mungu.
Sanduku la Mwenyezi Mungu lilibakia huko Kiriath-Yearimu kwa muda mrefu, jumla ya miaka ishirini.
Nao watu wote wa Israeli wakamrudia Mwenyezi Mungu.
Kisha Mfalme Daudi akaambiwa, "Mwenyezi Mungu ameibariki nyumba ya Obed-Edomu pamoja na kila alicho nacho, kwa sababu ya Sanduku la Mungu." Basi Daudi akateremka na kulipandisha Sanduku la Mungu kutoka nyumba ya Obed-Edomu hadi Mji wa Daudi kwa shangwe. Wale waliokuwa wamebeba Sanduku la Mwenyezi Mungu walipotembea hatua sita, Daudi alitoa dhabihu fahali na ndama aliyenoneshwa. Daudi, akiwa amevaa kizibau cha kitani, alicheza mbele za Mwenyezi Mungu kwa nguvu zake zote, wakati yeye na nyumba yote ya Israeli walipopandisha Sanduku la Mwenyezi Mungu kwa shangwe na sauti za tarumbeta.
Kisha Mfalme Sulemani akawaita mbele zake huko Yerusalemu wazee wa Israeli, viongozi wote wa makabila na wakuu wa jamaa za Waisraeli, ili walilete Sanduku la Agano la Mwenyezi Mungu kutoka Sayuni, Mji wa Daudi. Wanaume wote wa Israeli wakakusanyika kwa Mfalme Sulemani wakati wa sikukuu ya mwezi wa Ethanimu, ndio mwezi wa saba.
Wazee wote wa Israeli walipofika, makuhani wakajitwika lile Sanduku, nao wakalipandisha Sanduku la Mwenyezi Mungu, na Hema la Kukutania, pamoja na vyombo vyote vitakatifu vilivyokuwa ndani yake. Makuhani na Walawi wakavibeba, naye Mfalme Sulemani na kusanyiko lote la Israeli waliokuwa wamemzunguka wakasimama mbele ya hilo Sanduku, nao wakatoa dhabihu za kondoo na ng’ombe nyingi kiasi kwamba idadi yao haikuweza kuandikwa au kuhesabika.
Makuhani wakalileta Sanduku la Agano la Mwenyezi Mungu hadi mahali pake ndani ya mahali patakatifu sana humo Hekaluni, ndipo Patakatifu pa Patakatifu, na kuliweka chini ya mabawa ya makerubi. Makerubi yalitandaza mabawa yao juu ya mahali pa Sanduku la Agano na kutia kivuli Sanduku pamoja na mipiko yake ya kubebea. Mipiko hiyo ilikuwa mirefu sana kiasi kwamba ncha zake zilionekana kutoka Mahali Patakatifu mbele ya Patakatifu pa Patakatifu, lakini sio nje ya Mahali Patakatifu. Hiyo mipiko ipo hata leo. Ndani ya Sanduku hapakuwa na kitu kingine isipokuwa vile vibao viwili vya mawe ambavyo Musa aliviweka ndani yake huko Horebu, mahali Mwenyezi Mungu alipofanya agano na Waisraeli baada ya kutoka Misri.
Makuhani walipoondoka katika Mahali Patakatifu, wingu likajaza Hekalu la Mwenyezi Mungu. Nao makuhani hawakuweza kufanya huduma yao kwa sababu ya lile wingu, kwa kuwa utukufu wa Mwenyezi Mungu ulijaza Hekalu lake.
"Rudini, enyi watu msio waaminifu, kwa kuwa mimi ni mume wenu," asema Mwenyezi Mungu. "Nitawachagua ninyi, mmoja kutoka mji, na wawili kutoka ukoo, nami nitawaleta Sayuni. Kisha nitawapeni wachungaji wanaoupendeza moyo wangu, ambao watawaongoza kwa maarifa na ufahamu. Katika siku hizo, idadi yenu itakapokuwa imeongezeka sana katika nchi, watu hawatasema tena, ‘Sanduku la Agano la Mwenyezi Mungu,’ " asema Mwenyezi Mungu. "Halitaingia tena kwenye mawazo yao wala kukumbukwa, hawatalihitaji wala halitatengenezwa jingine.
Basi agano lile la kwanza lilikuwa na kanuni zake za kuabudu na pia patakatifu pake pa kidunia. Hema ilitengenezwa. Katika sehemu yake ya kwanza kulikuwa na kinara cha taa, meza na mikate iliyowekwa wakfu; hii sehemu iliitwa Mahali Patakatifu. Nyuma ya pazia la pili, palikuwa na sehemu iliyoitwa Patakatifu pa Patakatifu, ambapo palikuwa na yale madhabahu ya dhahabu ya kufukizia uvumba, na lile Sanduku la Agano lililofunikwa kwa dhahabu. Sanduku hili lilikuwa na gudulia la dhahabu lenye mana, ile fimbo ya Haruni iliyochipuka, na vile vibao vya mawe vya Agano. Juu ya lile Sanduku kulikuwa na makerubi wa Utukufu, wakikitia kivuli kiti cha rehema. Lakini hatuwezi kujadili vitu hivi kwa undani sasa.
Ndipo Hekalu la Mungu lililoko mbinguni likafunguliwa, na Sanduku la Agano lake likaonekana humo. Kukatokea miali ya radi, ngurumo, sauti za radi, tetemeko la ardhi na mvua kubwa ya mawe.