Publicidade

Arca de noé

Por Bíblia Online

A arca de Noé é história de salvação e fidelidade. Deus instruiu Noé a construir a arca para salvar sua família e os animais do dilúvio — exemplo supremo de obediência e fé.

Kwa hiyo Mungu akamwambia Nuhu, "Nitawaangamiza watu wote, kwa kuwa dunia imejaa ukatili kwa sababu yao. Hakika nitaangamiza watu pamoja na dunia. Kwa hiyo jitengenezee safina kubwa kwa mbao za mvinje; tengeneza vyumba ndani yake na uipake lami ndani na nje. Hivi ndivyo utakavyoitengeneza: Safina iwe na urefu wa dhiraa mia tatu, upana wake dhiraa hamsini, na kimo chake dhiraa thelathini. Itengenezee paa na umalizie safina kwa kuacha nafasi ya dhiraa moja juu. Weka mlango ubavuni mwa safina, na uifanye ya ghorofa ya chini, ya kati na ya juu.

Ndipo Mwenyezi Mungu akamwambia Nuhu, "Ingia katika safina, wewe na jamaa yako yote, kwa sababu katika kizazi hiki nimeona ya kuwa wewe ni mwenye haki.

Nuhu na mkewe, na wanawe na wake zao, wakaingia katika safina ili waepuke ile gharika. Jozi ya wanyama walio safi na walio najisi, ndege na viumbe vinavyotambaa ardhini, wa kiume na wa kike, walikuja kwa Nuhu, wakaingia katika safina kama Mungu alivyomwamuru Nuhu. Baada ya siku saba, maji ya gharika yakaja juu ya dunia.

Wanyama walioingia katika safina walikuwa wa kiume na wa kike, wa kila kiumbe chenye uhai kama Mungu alivyomwamuru Nuhu; ndipo Mwenyezi Mungu akamfungia ndani.

Kwa siku arobaini mafuriko yaliendelea kujaa duniani; maji yalivyozidi kuongezeka, yaliinua safina juu sana kutoka uso wa dunia. Maji yakajaa na kuongezeka sana juu ya dunia, na safina ikaelea juu ya maji.

Kila kitu chenye uhai juu ya uso wa nchi kilifutiliwa mbali; watu, wanyama pori, viumbe vinavyotambaa ardhini, na ndege warukao angani wakafutiliwa mbali toka duniani. Waliobaki ni Nuhu peke yake na wale waliokuwa pamoja naye ndani ya safina.

Maji yakaendelea kupungua taratibu katika dunia. Mwishoni mwa siku ya mia moja na hamsini, maji yakawa yamepungua. Na katika siku ya kumi na saba ya mwezi wa saba, safina ikatua katika milima ya Ararati.

Baada ya siku arobaini, Nuhu akafungua dirisha alilokuwa amelifanya katika safina, akamtoa kunguru, naye akawa akiruka kwenda na kurudi hadi maji yalipokwisha kukauka juu ya dunia. Kisha akamtoa hua ili aone kama maji yameondoka juu ya ardhi. Lakini hua hakupata mahali pa kutua, kwa kuwa maji yalienea juu ya uso wa dunia yote, kwa hiyo akarudi kwa Nuhu ndani ya safina. Nuhu akanyoosha mkono akamchukua yule hua, akamrudisha ndani ya safina. Nuhu akangojea siku saba zaidi, kisha akamtoa tena hua kutoka safina. Jioni hua aliporudi kwa Nuhu alikuwa amebeba jani bichi la mzeituni lililochumwa wakati ule ule katika mdomo wake! Ndipo Nuhu akajua ya kuwa maji yameondoka juu ya dunia. Akangojea siku saba zaidi na akamtuma tena hua, lakini wakati huu hua hakurudi tena kwa Nuhu.

Kufikia siku ya kwanza ya mwezi wa kwanza wa mwaka wa mia sita na moja (601) wa maisha ya Nuhu, maji yalikuwa yamekauka duniani. Kisha Nuhu akatoa kifuniko juu ya safina, akaona ya kuwa uso wa ardhi ulikuwa umekauka.

Ndipo Mungu akamwambia Nuhu, "Toka katika safina, wewe na mkeo, na wanao na wake zao. Utoe nje kila aina ya kiumbe hai aliye pamoja nawe, wakiwamo ndege, wanyama na viumbe vyote vinavyotambaa ardhini, ili wakazae, na kuongezeka na kuijaza tena dunia."

Ndipo Mungu akamwambia Nuhu na wanawe pamoja naye: "Sasa mimi ninaweka agano langu nanyi, pamoja na uzao wenu baada yenu, pia na kila kiumbe hai kilichokuwa pamoja nanyi: ndege, mifugo, na wanyama pori wote, wale wote waliotoka katika safina pamoja nanyi: kila kiumbe hai duniani. Ninaweka agano nanyi: Kamwe uhai hautafutwa tena kwa gharika; kamwe hakutakuwa tena gharika ya kuangamiza dunia."

Nimeweka upinde wangu wa mvua mawinguni, nao utakuwa ishara ya agano nifanyalo kati yangu na dunia.

Kwa imani, Nuhu alipoonywa na Mungu kuhusu mambo ambayo hayajaonekana bado, kwa kumcha Mungu alitengeneza safina ili kuokoa jamaa yake. Kwa imani yake aliuhukumu ulimwengu na akawa mrithi wa haki ipatikanayo kwa imani.

roho ambazo zamani hazikutii, wakati ule uvumilivu wa Mungu ulipokuwa ukingoja katika siku za Nuhu, wakati wa kujenga safina, ambamo watu wachache tu, yaani watu wanane, waliokolewa ili wasiangamie kwa gharika. Nayo maji hayo ni kielelezo cha ubatizo ambao sasa unawaokoa ninyi pia: si kwa kuondoa uchafu kwenye mwili, bali kama ahadi ya dhamiri safi kwa Mungu. Inatuokoa kupitia kwa ufufuo wa Isa Al-Masihi. Yeye ameingia mbinguni na amekaa mkono wa kuume wa Mungu; nao malaika, mamlaka na nguvu zote zimetiishwa chini yake.

Kama ilivyokuwa wakati wa Nuhu, ndivyo itakavyokuwa kuja kwake Mwana wa Adamu. Kwa maana siku zile kabla ya gharika, watu walikuwa wakila na kunywa, wakioa na kuolewa, hadi siku ile Nuhu alipoingia katika safina. Nao hawakujua lolote hadi gharika ilipokuja ikawakumba wote. Hivyo ndivyo itakavyokuwa atakapokuja Mwana wa Adamu. Watu wawili watakuwa shambani, naye mmoja atatwaliwa na mwingine ataachwa. Wanawake wawili watakuwa wanasaga kwa kinu cha mkono, naye mmoja atatwaliwa na mwingine ataachwa.

Seja o primeiro
Bíblia Online Bíblia Online

Bíblia Online • Versão: 2026-07-05_19-25-13-