Pular para o conteúdo
Publicidade

Ezekieli 30

Maombolezo Kwa Ajili Ya Misri

1 Neno la Bwana likanijia kusema: 2 "Mwanadamu, toa unabii na useme: Hili ndilo Bwana Mwenyezi asemalo:

" Ombolezeni ninyi na mseme,

"Ole wa siku ile!"

3 Kwa kuwa siku ile imekaribia,

siku ya Bwana imekaribia,

siku ya mawingu,

siku ya maangamizi kwa mataifa.

4 Upanga utakuja dhidi ya Misri,

nayo maumivu makuu yataijia Ethiopia.

Mauaji yatakapoangukia Misri,

utajiri wake utachukuliwa

na misingi yake itabomolewa.

5 Kushi30:5 Kushi ndiyo Ethiopia. na Putu, Ludi na Arabia yote, Libya30:5 Libya ndiyo Kubu. na watu wa nchi ya Agano watauawa kwa upanga pamoja na Misri.

6 " Hili ndilo Bwana asemalo:

" Wale walioungana na Misri wataanguka

na kiburi cha nguvu zake kitashindwa.

Kutoka Migdoli hadi Aswani,

watauawa ndani yake kwa upanga,

asema Bwana Mwenyezi.

7 " Hizo nchi zitakua ukiwa

miongoni mwa nchi zilizo ukiwa,

nayo miji yao itakuwa magofu

miongoni mwa miji iliyo magofu.

8 Ndipo watakapojua kwamba mimi ndimi Bwana,

nitakapoiwasha Misri moto

na wote wamsaidiao watapondwa.

9 " Siku hiyo wajumbe watatoka kwangu kwa merikebu, ili kuwatia hofu Ethiopia, wakiwa katika hali yao ya kuridhika. Maumivu makali yatawapata siku ya maangamizi ya Misri, kwa kuwa hakika itakuja.

10 " Hili ndilo Bwana Mwenyezi asemalo:

" Nitakomesha makundi ya wajeuri ya Misri

kwa mkono wa Nebukadneza mfalme wa Babeli.

11 Yeye na jeshi lake, taifa lililo katili kuliko mataifa yote,

litaletwa ili kuangamiza nchi.

Watafuta panga zao dhidi ya Misri

na kuijaza nchi kwa waliouawa.

12 Nitakausha vijito vya Naili

na nitaiuza nchi kwa watu waovu,

kwa mkono wa wageni,

nitaifanya nchi ukiwa na kila kitu

kilichomo ndani yake.

Mimi Bwana nimenena haya.

13 " Hili ndilo Bwana Mwenyezi asemalo:

" Nitaangamiza sanamu

na kukomesha vinyago katika Memfisi30:13 Kiebrania ni Nofu.

Hapatakuwepo tena na mkuu katika nchi ya Misri,

nami nitaeneza hofu katika nchi nzima.

14 Nitaifanya Pathrosi30:14 Pathrosi ni Misri ya Juu. kuwa ukiwa

na kuitia moto Soani,

nami nitaipiga kwa adhabu Thebesi30:14 Thebesi kwa Kiebrania ni No (au No-Amoni), mji katika Misri.

15 Nitaimwaga ghadhabu yangu juu ya Pelusiumu,30:15 Kiebrania ni Sini.

ngome ya Misri,

nami nitakatilia mbali

makundi ya wajeuri wa Thebesi.

16 Nitaitia moto nchi ya Misri;

Pelusiumu itagaagaa kwa maumivu makuu.

Thebesi itachukuliwa na tufani,

Memfisi itakuwa katika taabu daima.

17 Wanaume vijana wa Oni30:17 Yaani Heliopoli (Mji wa Jua). na wa Pi-Besethi30:17 Yaani Bubasti.

wataanguka kwa upanga

nayo hiyo miji itatekwa.

18 Huko Tahpanhesi mchana utatiwa giza

nitakapovunja kongwa la Misri;

hapo kiburi cha nguvu zake kitakoma.

Atafunikwa na mawingu

na vijiji vyake vitatekwa.

19 Kwa hiyo nitaipiga Misri kwa adhabu,

nao watajua kuwa Mimi ndimi Bwana.’ "

20 Katika mwaka wa kumi na moja, mwezi wa kwanza, siku ya saba, neno la Bwana likanijia kusema: 21 "Mwanadamu, nimevunja mkono wa Farao mfalme wa Misri. Haukufungwa ili upone au kuwekewa kipande cha ubao ili upate nguvu za kuweza kuchukua upanga. 22 Kwa hiyo hili ndilo Bwana Mwenyezi asemalo: Mimi ni kinyume na Farao mfalme wa Misri. Nitavunja mikono yake yote miwili, ule mkono ulio mzima pia na ule uliovunjika na kuufanya upanga uanguke toka mkononi mwake. 23 Nitawatawanya Wamisri miongoni mwa mataifa na kuwafukuza huku na huko katika nchi zote. 24 Nitaitia nguvu mikono ya mfalme wa Babeli na kuutia upanga wangu mkononi mwake, lakini nitavunja mikono ya Farao, naye atalia kwa huzuni mbele yake kama mtu aliyetiwa jeraha la kumfisha. 25 Nitaitia nguvu mikono ya mfalme wa Babeli, lakini mikono ya Farao italegea. Ndipo watakapojua kwamba Mimi ndimi Bwana, nitakapoutia upanga wangu mkononi mwa mfalme wa Babeli, naye ataunyoosha dhidi ya Misri. 26 Nitawatawanya Wamisri miongoni mwa mataifa na kuwafukuza huku na huko katika nchi mbalimbali. Ndipo watakapojua kwamba Mimi ndimi Bwana."

Estes versículos te tocaram? Ore agora!

+581 estão orando agora.

Junte-se à corrente de oração.

Veja também