3 Baada ya muda Kaini akaleta baadhi ya mazao ya shamba kama sadaka kwa Bwana. 4 Lakini Abeli akaleta fungu nono kutoka baadhi ya wazaliwa wa kwanza wa mifugo yake. Bwana akamkubali Abeli pamoja na sadaka yake, 5 lakini Mungu hakumkubali Kaini pamoja na sadaka yake. Kwa hiyo Kaini akakasirika sana, uso wake ukawa na huzuni.
6 Kisha Bwana akamwambia Kaini, "Kwa nini umekasirika? Kwa nini uso wako una huzuni? 7 Ukifanya lililo sawa, je, hutakubalika? Lakini usipofanya lililo sawa, dhambi inakuvizia mlangoni mwako, inakutamani wewe, lakini inakupasa uishinde."