1 Hili ndilo neno lililomjia Yeremia kutoka kwa Bwana: 2 "Shuka uende mpaka nyumba ya mfinyanzi, nami huko nitakupa ujumbe wangu." 3 Kwa hiyo nikashuka mpaka kwenye nyumba ya mfinyanzi, nikamkuta akifinyanga kwa gurudumu lake. 4 Lakini chombo alichokuwa akikifinyanga kutokana na udongo kilivunjika mikononi mwake, hivyo mfinyanzi akakifanya kuwa chombo kingine, umbo jingine kama vile ilivyoonekana vyema kwake yeye.
5 Kisha neno la Bwana likanijia kusema: 6 "Ee nyumba ya Israeli, je, siwezi kuwafanyia kama huyu mfinyanzi afanyavyo?" asema Bwana. "Kama vile udongo ulivyo katika mikono ya mfinyanzi, ndivyo mlivyo katika mkono wangu, ee nyumba ya Israeli.