Publicidade

Zacarias 13

Kutakaswa Dhambi

1 "Katika siku hiyo, chemchemi itafunguliwa kwa nyumba ya Daudi na wakazi wa Yerusalemu, kuwatakasa dhambi na unajisi.

2 "Katika siku hiyo, nitayakatilia mbali majina ya sanamu kutoka nchi, nayo hayatakumbukwa tena," asema Bwana Mwenye Nguvu Zote. "Nitaondoa manabii wao pamoja na roho ya uchafu katika nchi. 3 Ikiwa yupo yeyote atakayeendelea kutabiri, baba yake na mama yake waliomzaa watamwambia, ‘Ni lazima ufe, kwa sababu umesema uongo kwa jina la Bwana.’ Atakapotabiri, wazazi wake mwenyewe watampasua tumbo.

4 "Katika siku hiyo, kila nabii ataaibika kwa maono ya unabii wake. Hatavaa vazi la kinabii la nywele ili apate kudanganya watu. 5 Atasema, ‘Mimi sio nabii. Mimi ni mkulima; ardhi imekuwa kazi yangu tangu ujana wangu.’ 6 Ikiwa mtu atamuuliza, ‘Majeraha haya yaliyo mwilini mwako ni ya nini?’ Atajibu, ‘Ni majeraha niliyoyapata katika nyumba ya rafiki zangu.’

Mchungaji Apigwa, Nao Kondoo Watawanyika

7 "Amka, ee upanga, dhidi ya mchungaji wangu,

dhidi ya mtu aliye karibu nami!"

asema Bwana Mwenye Nguvu Zote.

"Mpige mchungaji,

nao kondoo watatawanyika,

nami nitageuza mkono wangu

dhidi ya walio wadogo,

8 katika nchi yote," asema Bwana,

"theluthi mbili watapigwa na kuangamia;

hata hivyo theluthi moja watabaki ndani yake.

9 Hii theluthi moja nitaileta katika moto;

nitawasafisha kama fedha isafishwavyo

na kuwajaribu kama dhahabu.

Wataliitia Jina langu

nami nitawajibu;

nitasema, ‘Hawa ni watu wangu,’

nao watasema, ‘Bwana ni Mungu wetu.’ "

Veja também

Publicidade
Bíblia Online Bíblia Online

Bíblia Online • Versão: 2026-06-16_06-50-08-