Kuishi kwa ajili ya Mwenyezi Mungu
1 Kwa hiyo, kwa kuwa Al-Masihi aliteswa katika mwili wake, ninyi nanyi jivikeni nia hiyo hiyo kwa maana mtu aliyekwisha kuteswa katika mwili ameachana na dhambi. 2 Kwa hivyo, haishi maisha yake yaliyobaki hapa duniani ili kutimiza tamaa mbaya za wanadamu, bali anaishi ili kutimiza mapenzi ya Mungu. 3 Kwa maana wakati uliopita, mmetumia muda mwingi mkifanya yale wapagani hupenda kutenda: wakiishi katika uasherati, tamaa mbaya, ulevi, karamu za ulafi, vileo, ngoma mbaya, na ibada chukizo za sanamu. 4 Wao hushangaa kwamba ninyi hamjiingizi pamoja nao katika maisha yao ya uovu uliopita kiasi, nao huwatukana ninyi. 5 Lakini itawapasa wao kutoa maelezo kwake yeye aliye tayari kuwahukumu walio hai na waliokufa.