45 Daudi akamwambia yule Mfilisti. "Wewe unanijia na upanga, mkuki na fumo, lakini mimi ninakujia kwa jina la Mwenyezi Mungu, Mungu wa majeshi ya mbinguni, Mungu wa majeshi ya Israeli, ambaye wewe umemtukana. 46 Siku hii Mwenyezi Mungu atakutia mkononi mwangu, nami nitakupiga na kukukata kichwa chako. Leo nitawapa ndege wa angani na wanyama wa nchi mizoga ya jeshi la Wafilisti, nayo dunia yote itajua kuwa yuko Mungu katika Israeli. 47 Wale wote waliokusanyika hapa watajua kuwa Mwenyezi Mungu haokoi kwa upanga wala kwa mkuki; kwa kuwa vita ni vya Mwenyezi Mungu, naye atawatia ninyi wote mikononi mwetu."