10 Basi wakafanya hivyo. Wakachukua ng’ombe wawili wa aina hiyo, wakawafungia hilo gari la kukokotwa, nao ndama wao wakawekwa zizini. 11 Wakaliweka Sanduku la Mwenyezi Mungu juu ya hilo gari la kukokotwa pamoja na lile kasha lenye ile mifano ya panya wa dhahabu na ya majipu ya dhahabu. 12 Kisha hao ng’ombe wakaenda moja kwa moja kuelekea Beth-Shemeshi, wakishuka bila kugeuka kuume au kushoto, huku wakilia njia yote. Watawala wa Wafilisti waliwafuata hao ng’ombe hadi mpakani mwa Beth-Shemeshi.
13 Wakati huu watu wa Beth-Shemeshi walikuwa wakivuna ngano yao huko bondeni, walipoinua macho yao na kuona lile Sanduku, wakafurahi kuliona. 14 Lile gari la kukokotwa lilikuja kwenye shamba la Yoshua wa Beth-Shemeshi, nalo likasimama kando ya mwamba mkubwa. Watu wakapasua mbao za lile gari la kukokotwa na kutoa dhabihu wale ng’ombe kuwa sadaka ya kuteketezwa kwa Mwenyezi Mungu. 15 Walawi walilishusha Sanduku la Mwenyezi Mungu, pamoja na lile kasha lililokuwa na vile vitu vya dhahabu na kuviweka juu ya ule mwamba mkubwa. Siku ile watu wa Beth-Shemeshi wakatoa sadaka za kuteketezwa na dhabihu kwa Mwenyezi Mungu.