Mungu wa faraja yote
3 Ahimidiwe Mungu na Baba wa Bwana wetu Isa Al-Masihi, Baba wa huruma na Mungu wa faraja yote. 4 Yeye hutufariji katika taabu zetu, ili tuweze kuwafariji walio katika taabu yoyote kwa faraja ambayo sisi wenyewe tumepokea kutoka kwa Mungu. 5 Kama vile mateso ya Al-Masihi yanavyozidi maishani mwetu, hivyo ndivyo faraja yetu inavyofurika kupitia kwa Al-Masihi. 6 Ikiwa tunataabika, ni kwa ajili ya faraja na wokovu wenu; tukifarijiwa, ni kwa ajili ya faraja yenu, iwaleteayo saburi ya mateso yale yale yanayotupata. 7 Nalo tumaini letu kwenu ni thabiti, kwa sababu tunajua kwamba kama vile mnavyoshiriki mateso yetu, ndivyo pia mnavyoshiriki faraja yetu.