Walimu wa uongo na uangamizi wao
1 Lakini pia waliinuka manabii wa uongo miongoni mwa watu, kama watakavyokuwako walimu wa uongo miongoni mwenu. Wataingiza mafundisho yasiyopatana na kweli kwa siri, hata kumkana Bwana Mungu Mwenyezi wa pekee aliyewanunua, na hivyo kujiletea wenyewe maangamizi ya haraka. 2 Nao wengi watafuata njia zao potovu, na kwa ajili yao njia ya kweli itatukanwa. 3 Nao katika tamaa zao mbaya, walimu hawa watajipatia faida kwenu kwa hadithi walizotunga wenyewe. Lakini hukumu imekwisha kutangazwa dhidi yao tangu zamani, wala uangamivu wao haujalala usingizi.