10 Baada ya Paulo kuona maono haya, tulijiandaa kwa haraka kuondoka kwenda Makedonia tukiwa tumesadiki kuwa Mungu alikuwa ametuita kuhubiri Injili huko.
Kuokoka kwa Lidia
11 Tukasafiri kwa meli kutoka Troa na kwenda moja kwa moja hadi Samothrake, na kesho yake tukafika Neapoli. 12 Kutoka huko tukasafiri hadi Filipi, mji mkuu wa jimbo hilo la Makedonia, uliokuwa koloni ya Warumi. Nasi tukakaa huko siku kadhaa.
13 Siku ya Sabato tukaenda nje ya lango la mji kando ya mto, ambapo tulitarajia kupata mahali pa kufanyia maombi. Tukaketi, tukaanza kuongea na baadhi ya wanawake waliokuwa wamekusanyika huko. 14 Mmoja wa wale wanawake waliotusikiliza aliitwa Lidia, mfanyabiashara wa nguo za zambarau, raia wa mji wa Thiatira, aliyekuwa mcha Mungu. Mwenyezi Mungu akaufungua moyo wake akaupokea ujumbe wa Paulo. 15 Basi alipokwisha kubatizwa yeye na watu wa nyumba yake, alitukaribisha nyumbani mwake, akisema, "Kama mmeona kweli mimi nimemwamini Bwana Isa, karibuni mkae nyumbani mwangu." Naye akatushawishi.
Paulo na Sila watiwa gerezani
16 Siku moja, tulipokuwa tukienda mahali pa kusali, tulikutana na mjakazi aliyekuwa na pepo wa uaguzi. Naye alikuwa amewapa mabwana zake mapato makubwa ya fedha kwa ubashiri. 17 Huyu mjakazi alikuwa akimfuata Paulo na sisi akipaza sauti na kusema, "Watu hawa ni watumishi wa Mungu Aliye Juu Sana, wao wanawatangazieni njia ya wokovu."