Paulo na Sila watiwa gerezani
16 Siku moja, tulipokuwa tukienda mahali pa kusali, tulikutana na mjakazi aliyekuwa na pepo wa uaguzi. Naye alikuwa amewapa mabwana zake mapato makubwa ya fedha kwa ubashiri. 17 Huyu mjakazi alikuwa akimfuata Paulo na sisi akipaza sauti na kusema, "Watu hawa ni watumishi wa Mungu Aliye Juu Sana, wao wanawatangazieni njia ya wokovu." 18 Akaendelea kufanya hivi kwa siku nyingi, lakini Paulo akiwa ameudhika sana, akageuka na kumwambia yule pepo mchafu, "Ninakuamuru katika jina la Isa Al-Masihi, umtoke!" Yule pepo mchafu akamtoka mara hiyo.
19 Basi mabwana wa yule mjakazi walipoona kuwa tumaini lao la kuendelea kujipatia fedha limetoweka, wakawakamata Paulo na Sila wakawaburuta hadi sokoni mbele ya viongozi wa mji. 20 Baada ya kuwafikisha mbele ya mahakimu wakawashtaki wakisema, "Hawa watu wanaleta ghasia katika mji wetu, nao ni Wayahudi. 21 Wanafundisha desturi ambazo sisi raia wa Rumi hatuwezi kuzikubali au kuzitimiza."
22 Umati wa watu wakajiunga kuwashambulia Paulo na Sila, na wale mahakimu wakaamuru wavuliwe nguo zao na wapigwe mijeledi. 23 Baada ya kuwapiga sana, wakawatupa gerezani na kumwagiza mkuu wa gereza awalinde kikamilifu. 24 Kufuata maelekezo haya, yule mkuu wa gereza akawaweka katika chumba cha ndani sana mle gerezani, na akawafunga miguu yao kwa minyororo.
25 Ilipokaribia usiku wa manane, Paulo na Sila walikuwa wakiomba na kuimba nyimbo za kumsifu Mungu, nao wafungwa wengine walikuwa wakiwasikiliza. 26 Ghafula pakatokea tetemeko kubwa la ardhi, hata msingi wa gereza ukatikisika. Mara milango ya gereza ikafunguka na ile minyororo iliyowafunga kila mmoja ikafunguka. 27 Yule mkuu wa gereza alipoamka na kuona milango ya gereza iko wazi, akachomoa upanga wake akataka kujiua, akidhani ya kuwa wafungwa wote wametoroka. 28 Lakini Paulo akapaza sauti kwa nguvu, akisema, "Usijidhuru kwa maana sisi sote tuko hapa!"
29 Yule askari wa gereza akaagiza taa ziletwe, akaingia ndani ya kile chumba cha gereza, akapiga magoti akitetemeka mbele ya Paulo na Sila. 30 Kisha akawaleta nje akisema, "Bwana zangu, nifanye nini nipate kuokoka?"
31 Wakamjibu, "Mwamini Bwana Isa Al-Masihi, nawe utaokoka, pamoja na watu wa nyumbani mwako." 32 Wakamwambia neno la Bwana Isa, yeye pamoja na wote waliokuwa nyumbani mwake. 33 Wakati ule ule, yule mkuu wa gereza akawachukua, akawaosha majeraha yao, kisha akabatizwa yeye pamoja na wote waliokuwa nyumbani mwake bila kuchelewa. 34 Akawapandisha nyumbani mwake akawaandalia chakula, yeye pamoja na nyumba yake yote wakafurahi sana kwa kuwa sasa walikuwa wamemwamini Mungu.
35 Kulipopambazuka wale mahakimu wakawatuma maafisa wao kwa mkuu wa gereza wakiwa na agizo linalosema, "Wafungue wale watu, waachie waende zao." 36 Mkuu wa gereza akamwambia Paulo "Mahakimu wameagiza niwaachie huru, kwa hiyo tokeni na mwende zenu kwa amani."
37 Lakini Paulo akawaambia wale maafisa, "Wametupiga hadharani bila kutufanyia mashtaka na kutuhoji, nao wakatutupa gerezani, hata ingawa sisi ni raia wa Rumi. Nao sasa wanataka kututoa gerezani kwa siri? Hapana! Wao na waje wenyewe watutoe humu gerezani."
38 Wale maafisa wakarudi na kuwaambia wale mahakimu maneno haya, wakaogopa sana walipofahamu kuwa Paulo na Sila ni raia wa Rumi. 39 Kwa hiyo wakaja wakawaomba msamaha, wakawatoa gerezani, wakawaomba waondoke katika ule mji. 40 Baada ya Paulo na Sila kutoka gerezani walienda nyumbani mwa Lidia, ambapo walikutana na waumini, wakawatia moyo, ndipo wakaondoka.