44 "Baba zetu walikuwa na lile Hema la Ushuhuda huko jangwani, ambalo lilitengenezwa kama Mungu alivyomwelekeza Musa, kulingana na kielelezo alichokiona. 45 Baada ya kupokea Hema, baba zetu waliingia nalo walipokuja na Yoshua wakati walimiliki nchi, Mungu alipoyafukuza mataifa mbele yao. Nalo lilidumu katika nchi hadi wakati wa Daudi, 46 ambaye alipata kibali kwa Mungu, naye akaomba kwamba ampatie Mungu wa Yakobo maskani. 47 Lakini Sulemani ndiye aliyemjengea Mungu nyumba.
48 "Hata hivyo, Yeye Aliye Juu Sana hakai kwenye nyumba zilizojengwa kwa mikono ya wanadamu. Kama nabii alivyosema:
49 " ‘Mbingu ni kiti changu cha enzi,
nayo dunia ni mahali pa kuweka miguu yangu.
Mtanijengea nyumba ya namna gani?
asema Mwenyezi Mungu.
Au mahali pangu pa kupumzikia patakuwa wapi?
50 Je, mkono wangu haukuumba vitu hivi vyote?’