2 Danieli akasema: "Katika maono yangu usiku nilitazama, na hapo mbele yangu kulikuwa na pepo kutoka pande nne za mbingu, zikivuruga bahari kuu. 3 Wanyama wanne wakubwa, kila mmoja tofauti na mwenzake, wakajitokeza kutoka bahari.
4 "Mnyama wa kwanza alifanana na simba, naye alikuwa na mabawa ya tai. Nikatazama hadi mabawa yake yalipong’olewa, naye akainuliwa katika nchi, akasimama kwa miguu miwili kama mwanadamu, naye akapewa moyo wa binadamu.
5 "Hapo mbele yangu kulikuwa na mnyama wa pili, aliyefanana na dubu. Upande wake mmoja alikuwa ameinuka, na alikuwa na mbavu tatu katika kinywa chake kati ya meno yake. Akaambiwa, ‘Amka, ule nyama, ushibe!’
6 "Baada ya huyo, nilitazama, na mbele yangu kulikuwa na mnyama mwingine, aliyefanana na chui. Juu ya mgongo wake alikuwa na mabawa manne kama ya ndege. Mnyama huyu alikuwa na vichwa vinne, naye akapewa mamlaka ya kutawala.
7 "Baada ya huyo, katika maono yangu usiku nilitazama, na mbele yangu kulikuwa na mnyama wa nne, mwenye kutisha na kuogofya, tena mwenye nguvu nyingi. Alikuwa na meno makubwa ya chuma; akapondaponda na kuangamiza wahanga wake, na kukanyaga chini ya nyayo zake chochote kilichosalia. Alikuwa tofauti na wanyama wote waliotangulia, naye alikuwa na pembe kumi.