Kuabudu miungu mingine
1 Kama nabii, au yule anayetabiri kupitia ndoto, akijitokeza miongoni mwenu na akawatangazia ishara ya miujiza na ajabu, 2 ikiwa ishara au ajabu ya aliyozungumza ikatokea, naye akasema, "Na tufuate miungu mingine" (miungu ambayo hamjaifahamu) "na tuiabudu," 3 kamwe msiyasikilize maneno ya nabii wala mwota ndoto huyo. Mwenyezi Mungu, Mungu wenu, anawajaribu kuangalia kama mnampenda kwa moyo wote na kwa roho yote. 4 Ni Mwenyezi Mungu, Mungu wenu, ambaye mnapaswa kumfuata tena ni yeye mnapaswa kumheshimu. Shikeni maagizo yake na kumtii, mtumikieni na kushikamana naye.